WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mipango ya serikali kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es Salaam ina lengo la kuhakikisha kwamba barabara zote zinapitika mwaka mzima ili kurahisisha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
Waziri huyo ametoa maelezo hayo jana mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyekuwa na ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam jana.
Ulega alitoa mfano wa ujenzi wa Daraja la Jangwani alilosema kukamilika kwake kutaondoa adha ya kukatika kwa njia ya kutoka Magomeni kuelekea katikati ya jiji na kurejea kwa kusema jambo hilo sasa litakuwa historia
“Nikwambia tu mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Jangwani litakalokuwa na urefu sawa na viwanja vinne vya mpira itamaanisha mambo ya njia kufungwa kwa sababu ya mafuriko yatakuwa historia, alisema waziri huyo ambaye pia ni Mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga.
Waziri Ulega amemueleza Waziri Mkuu kwamba daraja la Jangwani lina urefu wa mita 390, upana wa mita 42.8 na kimo cha mita 15, na litakuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la mafuriko katika eneo hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na changamoto hiyo wakati wa mvua.
Kwenye ziara hiyo ya ukaguzi, Ulega alisema maboresho makubwa yanayoendelea jijini Dar es Salaam yanatokana na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona kwamba miundombinu inakuwa fursa kwa Watanzania badala ya kusababisha kero na ukosefu wa utu kwa wakazi wa jiji hilo.
Pamoja na mambo mengine, Mwigulu alikagua miradi ya ujenzi wa madaraja ya Mkwajuni na Kigogo, ambapo alionesha kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa na kwamba hatua zinazochukuliwa zinaonesha mabadiliko makubwa ya maendeleo ya jiji hilo.
Waziri huyo alitoa pia taarifa kuhusu ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi aliosema umeleta mapinduzi makubwa kwa wananchi, akibainisha kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana kuanzia Mbagala hadi Kariakoo ikiwa na mabasi yenye viwango vya kisasa, hali inayorahisisha usafiri na kupunguza adha iliyokuwepo hapo awali.
Ulega ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, ambapo katika siku chache zijazo baadhi ya maeneo yataanza kuhudumiwa na mabasi ya mwendokasi, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri jijini humo.
Amesema juhudi hizo zinafanyika chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kudhibiti mafuriko, ikiwemo mradi wa mifereji katika eneo la Boko Basihaya wenye thamani ya shilingi bilioni 57, ambao kwa sasa uko katika hatua ya manunuzi ya kumpata mkandarasi.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madaraja ya Mzinga, Mpiji Chini na Ununio, ambayo kwa pamoja inagharimu shilingi bilioni 46.5, ikilenga kupunguza na kuondoa kabisa athari za mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Kuhusu miradi ya madaraja ya Kigogo na Mkwajuni iliyokaguliwa, Ulega amesema inagharimu jumla ya shilingi bilioni 28 na inalenga kuboresha mtandao wa usafiri, kuondosha changamoto ya mafuriko pamoja na kuimarisha usalama kwa watumiaji wa barabara.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
