TRA YAKUSANYA TRILIONI 3.58 MWEZI MACHI 2026 PEKEE



Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 3.58 kwa mwezi Machi pekee sawa na ufanisi wa asilimia 107.6 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 3.32 makusanyo ambayo yamechangiwa na ukaribu uliopo baina ya Mamlaka hiyo na Walipakodi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda April 1, 2026 imeeleza kuwa Makusanyo hayo ya mwezi Machi yanapelekea TRA kuwa imekusanya kiasi cha kiasi cha shilingi trilioni 9.31 sawa na ufanisi wa asilimia 106.4 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 8.75, katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26 (Januari hadi Machi 2026). 

Makusanyo hayo ya kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26, ni sawa na ukuaji wa asilimia 23.6 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi trilioni 7.53 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Ufanisi wa makusanyo kwa mwezi Machi unapelekea TRA kuweza kuandika rekodi mpya za kipekee katika ukusanyaji wa mapato nchini Wastani wa Makusanyo kwa mwezi katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025/26 umefikia shilingi trilioni 3.10 ambacho ni kiasi cha juu kabisa ukilinganisha na wastani wa shilingi trilioni 2.51  kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/25.

TRA imeweza kurekodi Ukuaji chanya wa asilimia 23.6 katika kipindi cha Januari -Machi 2026, na imeweza kulifikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi 21 mfululizo kuanzia mwezi Julai 2024, mafanikio ambayo Mamlaka haijawahi yafikia toka ianzishwe. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa kipindi hicho chote, Mamlaka imeweza kuwa na Wastani wa ufanisi wa utendaji wa shilingi trilioni 2.87 kwa kila mwezi.

Ufanisi huu wa makusanyo katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2025/26 ni muendelezo kwa vitendo wa utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuhakikisha kuwa Mamlaka inaongeza makusanyo ya kodi kwa kuongeza hali ya ulipaji kodi kwa hiari nchini. 

Imeeleza kuwa Makusanyo yaliyokusanywa kwenye robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2025/26 ni sawa na ukuaji wa asilimia 114.1 ukilinganisha na kiasi cha shilingi trilioni 4.35 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho wakati Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani, mwaka 2020/21. 

Taarifa hiyo imeweka wazi sababu zilizochangia ufanisi huo wa juu katika makusanyo ya robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2025/26 kuwa ni Kuendelea kuboresha mahusiano na walipakodi kwenye Shughuli zote za Kiuchumi ili kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini. 

Aidha, TRA imeendelea kuboresha mahusiano na ushirikiano na Wizara, Taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na mashirika ya kimataifa katika kuhakikisha wote wanahamasisha na kushiriki katika ulipaji kodi kwa hiari, kulingana na sheria na miongozo nchini. 

Pia ni matokeo chanya ya kuanza kutumika kwa mfumo jumuishi wa usimamizi wa kodi za ndani (IDRAS) kuanzia tarehe 9 februari 2026 ambapo katika miezi miwili ya ufanyaji kazi wa IDRAS, mamlaka imeweza kusajili walipakodi 69,733 mwezi. 

Aidha kupitia IDRAS TRA imeunganishwa (System Integration) na mifumo ya taasisi mbalimbali 92 zikiwemo 63 za Serikali na 27 za binafsi ambapo muunganiko huo umeongeza uwazi na kuboresha ubadilishanaji wa taarifa kati ya TRA na Taasisi nyingine, huku kazi ya kuunganisha na taasisi zingine ikiendelea.

Kuimarisha usimamizi wa vyanzo vyote vya Forodha kupitia matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) ulioboreshwa ikiwa pamoja na kuongeza ufanisi katika uondoshaji wa mizigo kwa mwaka 2025/26 katika vituo vyote vya Forodha. 

Pia TRA itaendelea kusogeza huduma karibu na walipakodi ili kuhakikisha kuwa walipakodi wote wanatimiza majukumu yao yote bila ya changamoto zozote toka TRA ambapo hili limefanikishwa kupitia Dawati la Uwezeshaji Biashara nchini.

Aidha TRA inapenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa itaendelea kushirikiana na wananchi wote kwa ukaribu ili kuhakikisha kuwa lengo la makusanyo kwa mwaka huu wa fedha 2025/26 linafikiwa lote na hivyo kuiwezesha Serikali kuweza tekeleza mipango ya maendeleo kwa manufaa ya Taifa zima.

Post a Comment

Previous Post Next Post