NDEJEMBI AONGOZA KIKAO CHA KUWEKA MIKAKATI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOJA ZA WABUNGE.


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius J. Ndejembi, pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba wamekutana na Viongozi wa Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara kuweka mikakati mahsusi ya kuanza utekelezaji wa hoja na mapendekezo yaliyotolewa na Wabunge, pamoja na kujipanga kwa utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri Ndejembi na Naibu Waziri Salome wamekutana na Viongozi hao katika kikao cha kwanza cha kimkakati mara baada ya Bajeti kupitishwa, kilichowashirikisha Makatibu Wakuu, Makamishna, Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo, Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakuu wa Taasisi na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Nishati.

Katika kikao hicho, Waziri Ndejembi amewataka viongozi wa kila idara na vitengo vya Wizara pamoja na Taasisi zake, kila mmoja kujipanga kimkakati katika utekelezaji wa mambo yote yaliyoahidiwa kupitia Bajeti, pamoja na kutafuta majawabu na utekelezaji wa maoni na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge yaliyotolewa wakati wa kujadili Bajeti.

Aidha, Ndejembi ametoa wito kwa Watumishi wote kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kutimiza dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwahudumia wananchi na kuwafikishia huduma bora na maendeleo kupitia sekta ya nishati.

Post a Comment

Previous Post Next Post