Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 785 kwa ajili ya kufungua na kuboresha barabara zinazoelekea katika vijiji vipya 22 katika Jimbo la Ulyankulu , vikiwepo vijiji vya Nyasa, Itumbo, Mwahalaja, Upele na Miti Mitano.
Dkt. Dugange amesema hayo leo Aprili 14, 2026 Bungeni Jijini Dodoma kwa Niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati akijibu swali la Mhe. Japhael Masanja Lufungija Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu aliyetaka kujua ni lini Serikali itaongeza bajeti ya TARURA Wilaya ya Kaliua ili kufungua Barabara katika vijiji vipya 22 vilivyopo katika jimbo hilo.
Dkt. Dugange amefafanua kuwa, kupitia bajeti za miaka ya fedha 2021/22 hadi 2024/25, Serikali ilitekeleza jukumu la kufungua barabara mpya za vijijini 22 jimboni Ulyankulu na kuongeza kuwa, vijiji vilivyonufaika ni pamoja na Twigu, Nhw’ande, katika Barabara yaTwigu-Nhw’ande kilometa sita (6), Vijiji vya Taba, Imara, Ibapa, Keza, katika Barabara ya Taba-Imara-Keza kilometa nane (8), vijiji vya Usonga, Ikonongo, katika Barabara ya Usonga-King’wangoko kilometa 18.
Dkt. Dugange ameainisha kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga bajeti ya Shilingi Milioni 987 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika wilaya ya Kaliua na kuongeza kuwa, mwaka 2021/22 na kuendelea, bajeti hiyo imeongezeka hadi kufikia Shilingi Bilioni 4.3, sawa na ongezeko la asilimia 335.66.
Akizungumza kuhusu mtandao wa barabara unaomilikiwa na TARURA, Dkt. Dugange amesema kwamba Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Wilaya ya Kaliua unasimamia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,370.41. Kati ya hizo, kilometa 9.23 ni barabara za lami, kilometa 329.73 ni barabara za changarawe, na kilometa 1,031.45 ni barabara za udongo.
