Taasisi ya Doris Mollel kwa kushirikiana na Shirika la Global Fund, linatarajia kuanza kutekeleza mradi wa kusaidia kuwarejesha shule wasichana wa rika balehe walioondoka nje ya mfumo rasmi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ujauzito.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na taasisi hiyo katika mikoa 15 ndani ya halmashauri 47 chini ya ufadhili wa Global Fund na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita nchini ukilenga kuwawezesha wasichana katika rika balehe na wanawake wadogo waliokatisha shule kwa changamoto mbalimbali kurejea shuleni pamoja na kuwapeleka kwenye nyumba salama wale wanaokimbia matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye makazi yao.
Vilevile, Taasisi ya Doris Mollel imebainisha kwamba mradi huo utazishawishi baadhi ya halmashauri kuwa za mfano katika utoaji wa taulo kwa wasichana shuleni.
Hayo yamebainishwa jana Aprili 28, 2026 kwenye kikao kazi cha wadau na maofisa wa Serikali waliokutana kujadili namna ya kutekeleza mradi huo na kuleta matokeo chanya kwenye jamii na uendelevu wake baada ya ufadhili wa mradi kutamatika.
Akifungua kikao hicho, Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Afya, Paul John amesema wizara hiyo inatambua na kuthamini michango ya wadau katika utoaji wa huduma za Ukimwi na afua zingine.
"Afua hii ni muhimu kwa ulinzi wa mtoto, sisi kama Wizara ya Afya tunafahamu eneo la wasichana rika balehe bado liko nyuma katika kukabili maambukizi na linaongoza kwa maambukizi.
"Kundi hili ndilo linaongoza kwa maambukizi ya ukimwi na hivyo mikakati mikubwa isipotengenezwa ya kuhakikisha ulinzi wa msichana, Taifa litaangamia na hakutakuwa na Taifa la kesho," amesema.
Naye, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Doris Mollel amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuandaa mikutano zaidi ya minne kila mwaka yenye lengo la kujadili namna ya kutatua changamoto kwa vijana.
"Kupitia jukwaa hili na mashirika zaidi ya 100 huwa tunakutana na kujadili changamoto wanazokutana nazo vijana na namna ya kuzitatua ikiwemo upatikanaji wa vyombo rafiki kwa vijana, upatikanaji wa bidhaa za watoto wa kike kwa gharama nafuu na watoto wa kike waliopata ujauzito wanaotamani kurudi shule lakini wameshindwa," amesema.
Amesema kupitia mradi wanaokwenda kuutekeleza kwa kipindi cha miezi sita ukifadhiliwa na Shirika la Global Fund wa kuwezesha watoto wa kike waliopata mimba kurudi kwenye mfumo wa elimu na kuwapeleka wengine nyumba salama watashawishi halmashauri kuwezesha watoto wa kike kupata taulo.
Doris amesema mradi huo utatekelezwa katika mikoa 14 watashirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha mradi huo aliouita ni wa matumaini.
"Mtoto wa kike atakayeguswa na mradi huu, tunakwenda kurudisha tumaini la maisha yake tena, lakini pia kwa namna ambavyo hizi nyumba salama zinakwenda kutunza utu wa mtoto wa kike ni jukumu letu kuhakikisha watoto wa kike wanaishi kwenye maisha bora," amesema.
