WAZIRI MHE. ANGELLAH KAIRUKI AZINDUA MADUKA MAPYA 17 YA AIRTEL SMART SHOPS


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amezindua rasmi maduka 17 mapya ya Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania (Airtel Smart Shops) leo Machi 12, 2026 katika hafla iliyofanyika katika eneo la Goba Centre, mkoani Dar es Salaam, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kairuki aliipongeza Kampuni ya Airtel Tanzania pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Charles Kamoto, kwa kuendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za mawasiliano na kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi kupitia maduka ya kisasa.

Aliongeza kuwa uwekezaji huo unaonesha imani kubwa ya wawekezaji kwa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye Serikali yake imeendelea kuweka mazingira wezeshi yanayochochea ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Waziri Kairuki alibainisha kuwa Jiji la Dar es Salaam lina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa kwani ni kitovu cha biashara, uwekezaji, huduma za kifedha na ubunifu wa vijana, hivyo maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano katika jiji hilo yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa kidijitali.

“Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa 2024 - 2034 unaolenga kuifanya Tanzania kuwa Taifa linalotumia Teknolojia kama kichocheo kikuu cha Maendeleo ya Uchumi na Jamii, “ alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alisema kuwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi ni jambo la Msingi sana huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuthamini mchango huu na kwamba kupitia ushirikiano wa karibu na wadau wa sekta ya Mawasiliano, watanzania wengi zaidi watafikiwa na huduma za Mawasiliano na Teknolojia.

Post a Comment

Previous Post Next Post