Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva amewakaribisha watumishi wapya waliopangiwa kufanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na kuwaasa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Pia amewasisitiza kujituma, kufanya kazi kwa upendo na kudumisha ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe Victoria Mwanziva akizungumza wakati wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa ajira za mwaka 2024/2025 na 2025/2026 ambayo yamefanyika Machi 11, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Mhe. Mwanziva amesema mafanikio ya kila mtumishi yatategemea kiwango cha kujituma na uwajibikaji wake binafsi katika kutekeleza majukumu ya kazi.
Katika hatua nyingine, amesisitiza kuwa watumishi hao wanapaswa kujenga mahusiano mazuri mahali pa kazi, kufanya kazi kwa umoja, mshikamano na kujitathmini mara kwa mara ili kujiendeleza kitaaluma na kuboresha utendaji wao.
"Fanyeni kazi kwa upendo, mshikamano na jitihada. Kufanikiwa kwenu kutatokana na kujituma kwenu wenyewe, na juhudi hizo ndizo zitakazowatofautisha katika utendaji wa kazi zenu," amesema Mhe. Mwanziva.
Aidha, amesema Mkoa wa Lindi unaendelea kukua kiuchumi na kimkakati, akitaja utekelezaji wa mradi mkubwa wa gesi asilia wa LNG unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha kuanzia mwezi Juni, ambao utachochea fursa mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu katika Halmashauri ya Mtama, Ndg. Edwin Ngonyani amesema halmashauri imepokea jumla ya watumishi wapya takribani 144 katika kada mbalimbali ili kusaidia kupunguza upungufu wa watumishi uliokuwepo hususan katika sekta za afya na elimu.
