WANAWAKE WAJASIRIAMALI MTUMBA WAPEWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI


Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mh. Anthony Mavunde leo amefunga mafunzo na kugawa vyeti vya mafunzo kwa wanawake wajasiriamali wa Jimbo la Mtumba walioshiriki semina ya ujasiriamali iliyoratibiwa na Taasisi ya Azurite,Tree of Hope na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mtumba.

Mbunge Mavunde amewashukuru wadau hao kwa kuandaa mafunzo yenye lengo la kuwawezesha wanawake wa Mtumba ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zitasaidia katika kuwainua na kuwaimarisha kiuchumi.

Mbunge Mavunde ameeleza mafunzo haya yanalenga kuliwezesha kundi la wakina mama kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi kama ambavyo serikali chini ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan ilivyojipambanua kuwapatia fursa mbali mbali wanawake wa Tanzania.

Aidha, katika kuwaunga mkono wajasiriamali hao Mbunge Mavunde amewaahidi kuchangia Tsh 12m kwa ajili ya ununuzi wa malighafi za kutengenezea bidhaa mbalimbali. 

Akitoa maelezo ya awali,Mratibu wa Mafunzo hayo Bi. Fortunata Manyeresa amesema mafunzo hayo ya siku tatu ya kutengeneza bidhaa mbalimbali yametolewa kwa kufuata taratibu zote muhimu na kuhusisha wataalamu kutoka vyuo vya Ufundi nchini kwa lengo la kuongeza tija ya mafunzo hayo.

Naye Diwani wa Kata ya Chihanga Mh. Alice Kitendya akishukuru kwa niaba ya wajasiriamali wa kata za Chihanga,Hombolo Bwawani na Hombolo Makulu  amewataka wakina mama hao kuzingatia mafunzo waliyoyapata na kuyatumia vyema kujijenga kiuchumi.

Post a Comment

Previous Post Next Post