UZINDUZI WA KAMPENI YA UPANDAJI MITI VUNJO WAFANA, WANAFUNZI WAHIMIZWA KUCHUKUA WAJIBU WA UTUNZAJI


Kampeni ya upandaji miti katika Jimbo la Vunjo imezinduliwa rasmi na kufanyika kwa mafanikio, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Uzinduzi huo umeongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Godfrey Mzava, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa kwa uangalifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. 

Amesema ni vyema kila mwanafunzi anayekabidhiwa mti akawajibika kuutunza hadi anapomaliza masomo yake, hatua inayolenga kujenga utamaduni wa uwajibikaji katika jamii.

Kampeni hiyo imefanyika katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, yakiwemo Kata ya Mwika Kaskazini katika Shule ya Sekondari Mwika, Kata ya Makuyuni katika Shule ya Sekondari Mieresini, pamoja na Kata ya Kirua Vunjo Kusini katika Shule ya Amali Koresa Sekondari.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, kampuni ya Ernst & Young imetoa miche ya miti 500, ikiwa ni mchango wa sekta binafsi katika kusaidia maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Enock Zadock Koola, amewashukuru wadau wote walioshiriki na kuunga mkono kampeni hiyo huku akisema kuwa, ataendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kushirikiana na wadau mbalimbali kusambaza miche ya miti katika maeneo mengine ya jimbo.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalum kupitia Jumuiya ya Wazazi, Mhe. Dkt. Catherin Joachim, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya, Ndg. Hussein Jamal, pamoja na madiwani wa kata mbalimbali akiwemo Mhe. Dickson Tarimo (Makuyuni), Mhe. Samwel Shao (Mwika Kaskazini), Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Geoffrey Mkunde (Kirua Vunjo Kusini) na Diwani wa Viti Maalum, Mwl. Pamela Lazaro Chuwa.

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo imeendelea kusisitiza kuwa, kampeni hiyo ni endelevu na inahitaji ushirikiano wa wananchi, taasisi za elimu pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya ya muda mrefu kwa jamii na vizazi vijavyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post