Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kusisitiza jamii kuchangamkia fursa zilizopo mtandaoni kwenye zama hizi za kidijiti na kuzingatia matumizi sahihi na salama ya huduma na bidhaa za mawasiliano.
Hayo yameelezwa kupitia Dream FM 91.3 Mbeya, na Maafisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Bartholomeo Titus, Meneja wa TCRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, na Bw. Brian Kalinga, Afisa TEHAMA Mwandamizi, tarehe 24 Machi 2026.
Hii ni sehemu ya uzinduzi wa Kampeni ya Elimu kwa Umma iitwayo “FURSA SANA” ambayo ni mwendelezo wa jitihada za TCRA kuhakikisha jamii ya Tanzania inanufaika na maendeleo ya teknolojia na kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa Uchumi wa kidijiti unaotegemea TEHAMA. Jitihada hizi zinaakisi dira ya TCRA ambayo ni “Kuwa na Jamii iliyowezeshwa na Huduma Jumuishi na Endelevu za Mawasiliano”.
TCRA imetoa wito kwa jamii kuzichangamkia fursa kama vile kutangaza biashara kupitia mitandao, kupata elimu, kuongeza ujuzi, kutafuta ajira, kutengeneza mtandao (networking), pamoja na kuonesha vipaji vinavyoweza kuwa vyanzo vya ajira ya kudumu, na fursa nyingine nyingi
