TCRA YAADHIMISHA SIKU YA HAKI ZA MTUMIAJI DUNIANI MKOANI MTWARA


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeadhimisha siku ya Haki za Mtumiaji Duniani katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Kampasi ya Mtwara, tarehe 14 Machi, 2026.

Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ni Rasi wa Ndaki, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Kampasi Ya Mtwara Profesa Duwa Chengula. Katika hotuba ya ufunguzi, Profesa Duwa ametoa wito kwa washiriki kutumia huduma na bidhaa za mawasiiano ikiwemo teknolojia za kidijiti kama sehemu ya kupata maarifa, kushiriki mijadala ya kitaaluma, kutafuta nafasi za mafunzo kwa vitendo, kutafuta ajira na hata kuendeleza vipaji.

TCRA imeshirikiana na Chuo cha MUST kampasi ya Mtwara katika kuadhimisha siku ya haki za watumiaji duniani kwa lengo la kuongeza wigo wa ushirikishwaji wa wanafunzi ambao ni sehemu ya watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano, na wadau muhimu kwenye ujenzi wa Uchumi wa kidijiti unaotegemea TEHAMA.

Maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Bidhaa Salama, Watumiaji wenye Ujasiri”. Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama katika matumizi ya huduma na bidhaa za mawasiliano, kwa kuzingatia haki na wajibu wa watumiaji, pamoja na kuongeza uelewa, kuchukua tahadhari, na kuchagiza matumizi chanya ya fursa zilizopo.

Maadhimisho haya ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika jijini Tanga Machi 15, 2026 na kuratibiwa na Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF).

Post a Comment

Previous Post Next Post