NDEJEMBI AKUTANA NA IFC KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI TANZANIA


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Mary Porter leo Machi 25, 2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimelenga kujadili utekelezaji wa Mpango Mahususi wa Nishati wa Taifa (Mission 300) pamoja na ushirikishwaji wa sekta binafsi nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ndejembi ameieleza IFC mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Sita ya kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia MW 4,500 ikilinganishwa na MW 1,500 zilizokuwepo mwaka 2021.

Aidha Mhe. Ndejembi ameieleza IFC kazi inayoendelea kwa sasa ya kuunganisha umeme kwenye vijiji vyote 12,318 nchini ambapo ameeleza mafanikio hayo pia yametokana na ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa IFC Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Mary Porter ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika sekta ya nishati na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuziwezesha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya nishati.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Kamishna wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga pamoja na wataalamu kutoka taasisi zilizo chini ya wizara na wale wa IFC.

Post a Comment

Previous Post Next Post