MRADI WA TACTIC KUBORESHA MIUNDOMBINU MANISPAA YA MTWARA MIKINDANI


Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) chini ya mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) inalenga kubadilisha mandhari ya mkoa wa Mtwara kwa kujenga miundombinu mbalimbali itakayosaidia kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji pamoja kuondoa kero ya mafuriko katika makazi ya wananchi.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Bw. Rugembe Maiga ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo kwani utasaidia shughuli za kiuchumi na kijamii baada ya kukamilika.

"Mradi huu unakuja kama mkombozi kwenye Manispaa yetu, ujenzi wa stendi ya kisasa katika eneo la Chiputa utapendezesha mji wetu pia ujenzi wa mfereji wa maji utasaidia kuondoa maji katika makazi ya watu  na hii itasaidia katika kuongeza hadhi ya maeneo husika", amesema.

Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Mtwara Mhandisi Zuena Mvungi amesema kuwa licha ya mradi huo kuongeza mtandao wa barabara za lami kwa TARURA pia utagusa maisha ya wananchi hasa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kalakana ya wajasiriamali na ujenzi wa mfereji utakaosaidia kuondoa maji katika makazi ya wananchi hasa kipindi cha masika.

"Sisi kama TARURA tutahakikisha tunasimamia kwa umakini mradi huu ili ukamilike na kutoa huduma kwa wananchi kama yalivyo matarajio ya Serikali".

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa TACTIC kwa upande wa TARURA ambaye pia ni Meneja wa TARURA Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mhandisi Hatibu Nunu amesema kuwa, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Km 5.9, ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Chiputa, ujenzi wa Kalakana ya Wajasiriamali na ujenzi wa mfereji wenye urefu wa kilometa 1.7.

"Kupitia mradi huu wa TACTIC tunatarajia kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ya Manispaa yetu ikiwa ni pamoja na kujenga stendi ya kisasa itakayosaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja hasa wale watakaokuwa wanahusika katika kufanya shughuli za kibiashara", amesema.

Wakiongea kuhusu ujio wa mradi huo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani akiwemo Bi. Mariam Juma na Bw. Yusuph Namanoro amesema kuwa kutokana na mafuriko ya mara kwa mara hasa kipindi cha masika katika eneo la Kiangu, thamani ya viwanja na nyumba imekuwa ya hali ya chini lakini kwa ujenzi wa mfereji wa maji, thamani ya maeneo hayo itapanda maradufu.

Aidha, wameipongeza Serikali kwa kuleta mradi huo ambao licha ya kuondoa changamoto mbalimbali utasaidia kukuza uchumi wa Manispaa hiyo na kupendezesha mji.

Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaendelea kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuboresha maisha ya wananchi na kuondoa kero mbalimbali zilizokuwepo.

Post a Comment

Previous Post Next Post