Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Paul Walalaze amewashauri madereva wa bodaboda, bajaji na magari nchini kuhakikisha wanabeba risiti pindi wanaposafirisha mizigo ili kuepuka changamoto za sharia za forodha.
Wito huo ameutoa leo Tarehe 28, Machi, 2026 jijini Dar es salaam wakati akizungumza katika hafla ya kutoa tuzo za wanawake wafanyakazi na waliojiajiri sekta ya usafirishaji, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa na nyaraka halali za mizigo wanayoisafirisha.
CPA. Walalaze ameonya kuwa kwa mujibu wa sheria za forodha, iwapo mtu atasafirisha mzigo usio na nyaraka au ambao haujalipiwa kodi, hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi ya dereva, chombo cha usafiri pamoja na mmiliki.
“Mtu anaweza kukuambia uchukue mzigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini hakikisha unajiridhisha kuwa kuna nyaraka. Hata kama ni kwa njia ya simu, mwambie akutumie risiti,” amesisitiza Meneja Walalaze.
Amesema ni wajibu wao kuwa mabalozi wa utii wa sheria kwa kuhakikisha mizigo wanayobeba ina nyaraka halali ili kurahisiha shughuli zao za usafirishaji.
Aidha, amesema hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokea maoni ya wadau mbalimbali kuhusu maboresho ya kodi, hatua ambayo inalenga kumjengea mazingira Mtanzania awe sehemu ya sekta rasmi.
Amefafanua kuwa TRA imepewa jukumu la kuhakikisha inakusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya taifa, ambapo mapato hayo yamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi.
Ameongeza kuwa mapato ya kikodi yamegawanyika katika sehemu mbalimbali ikiwemo kodi za uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi kama China na Dubai, ambazo zinasimamiwa na Idara ya Forodha.
