KAMATI YA SIASA KAGERA YAKAGUA DARAJA LA KYANYABASA LILOWAHUDUMIA WANANCHI BAADA YA KERO YA MUDA MREFU


Serikali ya Rais Samia inajenga Daraja la Kisasa la Kyanyabasa la Bilioni 9.7 likifikia 90% likiunganisha zaidi ya nusu ya Wilaya ya Bukoba. Leo wananchi hakuna tena kulipia ukivuka._

Kamati ya Siasa ya CCM  ya Mkoa wa Kagera ikiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Ndugu Karim Amri imefanya ziara kwenye Tarafa ya Katerero, Wilaya ya Bukoba kukagua mradi mkubwa wa Daraja la Kisasa la Kyanyabasa linalojengwa kati ya Kata ya Bujugo na Kishogo likiunganisha zaidi ya nusu ya Wilaya ya Bukoba Vijijini. Ujenzi ukifikia zaidi ya 90%. 

Eneo hili limetesa wananchi miaka kwa miaka wengine wakipoteza maisha wakati wa kuvuka eneo hili lenye mto, lakini sasa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa Bilioni 9.7 kujenga Daraja hili la Kisasa kukatisha Mto Ngono na kuondoa usafiri wa mitumbwi na kivuko ambapo wananchi walikua wanalipia fedha kuvuka tena ikifika usiku kivuko kinafungwa.

Kamati ya Siasa imeridhishwa na ujenzi wake na kuishukuru Serikali ya Rais Samia kwa ukombozi huu mkubwa kwa wananchi ambapo sasa wanavuka bure bila kutumia mitumbwi wala kivuko cha kulipia.

Pia, Kamati ya Siasa ndani ya Tarafa ya Katerero ilitembelea ujenzi wa Ofisi ya CCM Wilaya ya Bukoba Vijijini inayojengwa kwenye Kata ya Kemondo ikijengwa kwa fedha binafsi na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Mhe. Jasson Rweikiza.

Pamoja nao, Kamati ya Siasa Mkoa iliambatana na Viongozi wa CCM Wilaya ya Bukoba Vijijini chini ya Mwenyekiti wake Ndugu Evarister Babyegeya, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima, Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Proscovia Mwambi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukoba Bi. Fatina Laay, Afisa Tarafa ya Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku na viongozi wengine mbalimbali.

Post a Comment

Previous Post Next Post