Takribani shilingi 6,650, 249,461 kutoka mfuko wa Wanayamapori wa Wizara ya Malisili na Utalii zimetumika kuimarisha uhifadhi wa Wanyamapori nchini.
Pamoja na mambo Mengine fedha hizo zinetumika katika ujenzi wa mabwawa ya maji katika mapori ya akiba, ununuzi wa Mikanda yenye visukuma mawimbi, kuwezesha sensa ya wanyamapori, miradi ya ujenzi wa maktaba na ofisi za taasisi.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya wahasibu wa kitengo cha fedha cha Wizara ya Maliasili na Utalii katika chuo cha Usimamizi wa wanyamapori Mweka, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori na Pori la Akiba Makuyuni.
Kiongozi wa Msafara huo Bwana John Komba amesema, shilingi 750,000,000 zilipelekwa katika chuo cha Usimamizi wa wanyapori Mweka kwa lengo la kuimarisha miundo mbinu ya kujifunzia kwa kujenga maktaba kubwa ya kisasa inayokidhi mahitaji ya chuo kwasasa kwani maabara iliyopo inaweza kuhudumia wanafunzi 80 pekee wakati chuo kina wanafunzi zaidi ya 1,500.
Aidha bwana Komba amesema, katika Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) wizara imepeleka kiasi ya shilingi 750,000,000 awamu ya kwanza kati ya shilingi 1,500,000,000 zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la makao makuu ya ofisi ya taasisi hiyo, aidha aliongeza kuwa utekelezaji huo unaendana na Falsafa ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita ya kazi na Utu ikiwa na maana ya kuboresha miundo mbinu ya sehemu za kazi.
Vilevile Bwana Komba amesema kiasi cha shilingi 3,999,999,461 zilitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ya sensa ya wanyamapori ambapo shughuli hiyo ilitekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI). Sensa ya wanyamapori ni muhimu kwa kubaini idadi, mgawanyo, na mwenendo wa spishi ili kuweka mikakati madhubuti ya uhifadhi. Pia inasaidia kutathmini afya ya mazingira, kupambana na ujangili, kurekebisha migogoro ya binadamu na wanyama, na kuongoza uwekezaji wa utalii.
Bwana Komba amesema kuwa kiasi cha shilingi 1,200,000,000 zilipelekwa katika Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa kumi ya maji katika mapori ya akiba ikiwa na lengo kupunguza uhaba wa maji wakati wa kiangazi ili kudhibiti wanyama kutokwenda kwenda kwenye maeneo yanayotumiwa na binadamu kwa ajili ya uhaba wa maji.
Aidha bwana Komba alisema kuwa lengo kuu la wahasibu kufanya ziara kwenye miradi hiyo ni kuona ufanisi wa matumizi ya fedha za miradi hiyo (Value for Money). Aidha ziara hizi husaidia kukagua ubora, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, na kuhakikisha malipo yanaendana na kazi iliyofanyika.
