NDEJEMBI: TANZANIA INA FURSA KUBWA YA KUENDELEZA NISHATI YA JOTOARDHI


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania imejidhatiti katika kuendeleza nishati ya jotoardhi ili kuhakikisha nchi inakuwa na nishati ya kutosha, nafuu na endelevu  inayotokana na vyanzo mchanganyiko lakini pia ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono malengo ya dunia ya kuelekea kwenye uzalishaji wa umeme unaotokana na nishati safi.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Januari 12, 2026 kwenye Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) katika Mkutano wa Mwaka wa Muungano wa Kimataifa wa Jotoardhi (Global Geothermal Alliance – GGA), unaofanyika Jijini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.

Waziri Ndejembi amesema ili kutekeleza dhamira hiyo Serikali imeweka mipango ya uzalishaji wa umeme wa jotoardhi katika Dira ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) na Mkataba wa Nchi kuhusu Masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi (NDCs).

Amesema Tanzania pia kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendeleza maeneo kadhaa ya kipaumbele ya jotoardhi ikiwemo Ngozi (MW 70), Songwe (MW 5–38), Kiejo-Mbaka (MW 60), Natron (MW 60) na Luhoi (MW 5), huku lengo likiwa ni kuwa na mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme wa megawati 130 ifikapo 2030 ambapo mtambo huo utaanza kwa kuzalisha megawati 30.

Ndejembi amesema kuwa kutokana na uwepo wa Bonde la Ufa, Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya jotoardhi vinavyoweza kuzalisha megawati 5,000 za umeme. Ametaja kuwa kuna maeneo 52 yenye viashiria vya jotoardhi ndani ya mikoa 16.

Katika mkutano wa IRENA, Waziri Ndejembi ameambatana na Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bakari Ameir, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma pamoja na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Nishati.

Post a Comment

Previous Post Next Post