KAIRUKI: MAGEUZI YA KIDIJITALI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb) ametembelea Kampuni ya Huduma za Taarifa za Kielektroniki ya China (China Electronic Information Services Co. - CEIS) na kupokelewa na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bw. Chen Wenhai katika Ofisi za Makao Makuu ya Kampuni hiyo zilizopo katika Jiji la Shenzhen nchini China. kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na.

Ziara hiyo ya Kikazi ilifanyika tarehe 22 Januari, 2026 ikilenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China kwa kubadilishana uzoefu na kuleta mabadiliko ya kidijitali kupitia teknolojia za kisasa. 

Waziri Kairuki alisema kuwa chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa kwa kuongeza huduma za intaneti yenye kasi, kuimarisha usalama wa mtandao, kukuza ujuzi na kujenga mazingira wezeshi kwa bunifu mbalimbali na teknolojia za kisasa. Mageuzi haya yamelenga kuhakikisha kila Mtanzania popote alipo anufaike na fursa kupitia huduma mbalimbali katika zama za kidijitali.

“Tunatambua fursa kubwa za ushirikiano katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Utengenezaji na uunganishaji wa vifaa vya TEHAMA, maonesho ya kikanda ya Vifaa vya Kielektroniki, kujenga uwezo kwa vijana wabunifu na wahandisi pamoja na huduma za wingu na suluhisho za kidijitali zitakazochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali,” alisema Waziri Kairuki.

Kampuni ya CEIS ni kampuni inayotambulika kimataifa katika sekta ya Vifaa vya Kielektroniki, miundombinu ya Kidijitali, usalama mtandao pamoja na utafiti na ubunifu wa teknolojia za kisasa kwenye sekta ya TEHAMA.

Serikali ya Tanzania na Kampuni ya CEIS zilisaini Hati ya Makubaliano mwezi Oktoba, 2024 ili kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kielektroniki, taarifa na uchumi wa kidijitali. Ambapo ushirikiano huu utaboresha utoaji wa huduma za umma na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post