Kamishna Uhifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro Abdul - Razaq Badru ametakiwa kuhakikisha hifadhi ya Ngorongoro inalindwa na kuhifadhiwa ili ikolojia yake istawi na kuendelea kuvutia watalii,kuhifadhi wanyamapori, misitu na viumbe hai wengine.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, jijini Arusha baada ya kumwapisha Kamishna huyo na kuizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Dkt. Kijaji amesema kuwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameonesha imani kubwa kwa Kamishna huyo, hivyo pamoja na mambo mengine anapaswa kuingoza vyema Mamlaka hiyo ili iweze kufikia matarajio yaliyokusudiwa hususani ya kufikia ya idadi ya watalii Milioni 8 kitaifa.
"Unapaswa uhakikishe huduma za malazi zinaendelea kuboreshwa kwa kuvutia uwekezaji utakaoongeza vitanda kutoka 1,555 hadi kufikia vitanda 2,586". Alisema Dkt. Kijaji.
Amesisitiza kuwa ni imani ya Wizara kuwa, baada ya kuapishwa kwake na kuvishwa cheo atazingatia maelekezo hayo katika kuhakikisha majukumu yote matatu ya Mamlaka hiyo anayafanyia kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, na ubunifu wa hali ya juu ili kurudisha hadhi ya Ngorongoro kama ambavyo ametekeleza katika kipindi cha miezi saba iliyopita tangu kuteukiwa kwake.
Akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo mpya, licha ya kuwapongeza, Dkt. Kijaji amewataka kuhakikisha wanaisimamia kikamilifu Taasisi hiyo kwa kutekeleza maelekezo ya Viongozi wa Serikali, masuala ya uhifadhi na utalii yaliyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amewaagiza kuhakikisha watendaji wa Taasisi wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakiongozwa na kauli ya Kazi na Utu.
Akiitambulisha Bodi hiyo mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, amesema kuwa, bodi hiyo inawajumbe licha ya taaluma zao lakini ni watunwenye uzoefu mkubwa katika nyanja mbalimbali hivyo ni anaamini kuwa watatoa mchango mkubwa katika kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
