Leo Disemba 24, 2025 ni siku Moja kabla ya Wakristo kote duniani kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mfalme wa amani- Rais Wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatimiza takribani siku 1,742 Miezi 57 na siku sita sawa na wiki 248 na siku sita madarakani.
Kabla mwaka haujaisha niseme kwamba athari za Rais Samia katika Miaka yake takribani mitano aliyokuwa madarakani ni nyingi, za kujaa na nyingine zisizopimika katika mizani ya kawaida. Moja kubwa, nimsifu na kumpongeza kwa uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya huduma za kijamii (afya, elimu na Maji).
"Kando ya huduma hizo, kuna ziada ya Tume yake ya haki jinai, matamanio na mpango wake wa kupatikana kwa Katiba mpya katika kipindi chake hiki, kurejesha tabasamu kwa Watanzania, Falsafa yake ya 4R pamoja na kutaka kuanza kwa mchakato wa maridhiano baada ya vurugu na ghasia za Oktoba 29, 2025 ni mambo yanayomtambulisha na kumtofautisha Dkt. Samia na Viongozi wengi duniani." Amesema Daniel Laizer, Mchambuzi na mwandishi wa Makala za siasa nchini.
Mwaka 2025 unaisha. Unaweza kuwa miongoni mwa miaka iliyobeba mitihani zaidi katika mawanda ya kisiasa nchini, kumeshuhudiwa mtikisiko mkubwa wa kisiasa, athari katika mshikamano wa Taifa, mambo yaliyoibua hoja ya haja ya upatanishi wa kitaifa. Lakini, mwaka huo huo kwa upande mwingine, umedhihirisha uwezo, maarifa na kipaji kikubwa cha kuwaunganisha watanzania alichopewa Dkt. Samia. umekuwa mwaka wa fursa za kiuchumi, marekebisho ya sera za ndani na nje na kuimarisha juhudi za kidiplomasia.
Kwa Afrika Mashariki, Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa mwendo mzuri wa kiuchumi. Ripoti za Benki ya Dunia na Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF), zinaonesha afya ya kifedha ya Tanzania inazidi kuimarika. Ukuaji wa Pato la Ndani la Taifa (GDP), kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ulivuka makisio ya asilimia 5.5 hadi kuwa asilimia 5.6. Sera za kifedha za Serikali ya Tanzania, zimewezesha mfumuko wa bei kugota asilimia 3.1. Sarafu ya Tanzania imeimarika. Dola ya Marekani inauzwa kwa Sh2,400 kutoka Sh2,800. Mapato ya ndani yameongezeka. Ripoti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Septemba 2025, ilionesha makusanyo ya mwezi ni Sh3.47 trilioni, kutoka Sh1.8 trilioni, ambazo Rais Samia alikuta serikali inakusanya wakati anaapishwa kwa mara ya kwanza kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021.
Yote hayo ukiyaweka kwenye kapu moja ni kwamba hutokea kutokana na sera nzuri za serikali kifedha. Mwandishi wa Makala Luqman Maloto anasema Duniani kote, ni vigumu watu kuandamana nyakati ambazo nchi yao inafanya vizuri kiuchumi. Mafanikio ya kiuchumi huakisi hali bora za watu, na upatikanaji wa uhakika wa huduma za kijamii. Imetokea Tanzania, mwezi mmoja kabla ya Oktoba 29, 2025, wananchi walikuwa wakilalamika huduma mbovu za mabasi yaendayo kasi, Dar es Salaam, kwa sababu yalikuwa machache.
Mabasi mapya, mengi na ya kisasa, yaliingizwa na kuanza kazi. Kero iliyokuwa inalalamikiwa ikaondoka. Oktoba 29, 2025, vijana waliyachoma mabasi moto mabasi hayo mapya ambayo yalikuwa mkombozi wa usafiri wa umma. Tafsiri ya matendo hayo ni tata. Nadharia ya vitendo hivyo ni zaidi ya moja.
"Jumuiya za Kimataifa zinaita ghasia za Oktoba 29, 2025 ni maandamano. Wapo watu wanahoji, aina gani ya maandamano yaliyojikita kushambulia mali za umma na za watu binafsi? Maandamano gani hayakuwa na mabango ya kuwasilisha ujumbe wa kile walichokitaka kitokee?" Anasema Bw. Maloto.
Mungu atutangulie Watanzania, atupe ufahamu, atupe chujio la kujua wema na wabaya kwa maisha yetu ni akinanani, zaidi tuungane pamoja kuwaombe wote wenye kutuwazia mema hasa Mimi na wewe GenZ. Kheri ya Krismasi na mwaka mpya.
