MSOVERA AWATAKA WAKUU WA VITENGO KUFANYA MAAMUZI YA PAMOJA NA KUIMARISHA UWAJIBIKAJI


Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Albert Msovera, amewataka Wakuu wa Vitengo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kujiona kama watatuzi wa changamoto za wananchi kwa kushirikiana, kufanya maamuzi ya pamoja na kudumisha umoja ili kuhakikisha maendeleo ya Mikoa yanapatikana kwa wakati.

Bw. Msovera ametoa wito huo wakati wa mafunzo ya uongozi na utendaji kazi kwa Wakuu wa Vitengo yaliyofanyika Jijini Dodoma, akisisitiza kuwa bila umoja, maamuzi ya pamoja na uwajibikaji wa Viongozi, Mikoa haitasonga mbele kimaendeleo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, amesema viongozi wa umma wana jukumu kubwa la kutatua migogoro na kero za wananchi kwa weledi na uadilifu, akisisitiza kuwa kushindwa kuwajibika kwa pamoja kunasababisha kuchelewesha maendeleo na kupunguza imani ya wananchi kwa Serikali.

“Sisi ndio watatuzi. Tukikosa kufanya maamuzi kwa pamoja na kudumisha umoja bila kuwajibika kwa pamoja, mikoa haitasonga mbele. Nendeni mkaangalie migogoro iliyopo na hakikisheni mnaitatua kwa maslahi ya wananchi,” amesisitiza Bw. Msovera.

Ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kushuka hadi ngazi ya wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuchukua hatua za haraka na sahihi katika kutatua migogoro, huku wakizingatia sheria, taratibu na misingi ya haki lakini pia kuimarisha mahusiano mazuri na wananchi kwa kuongeza tabasamu, lugha nzuri na heshima katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wao, Wakuu wa Vitengo walioshiriki mafunzo hayo wameahidi kuyatekeleza maelekezo yaliyotolewa kwa vitendo kwa kushirikiana, kufanya maamuzi ya pamoja, kushughulikia migogoro iliyopo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika mikoa yao.

Post a Comment

Previous Post Next Post