Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Jimbo la Uyole Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo Disemba 18, 2025 ameshiriki katika ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliyoifanya katika mkoa wa Mbeya.
Katika ziara hiyo Dkt. Tulia ametoa pole kwa Serikali kwa uharibifu wa mali za umma na mali binafsi katika vurugu zilizotokea Mwezi Oktoba, 2025.
Aidha, Dkt. Tulia amemuomba Waziri Mkuu ambaye Wizara ya TAMISEMI iliyopo chini yake kuipa kipaumbele Halmashari ya jiji la Mbeya akijumuisha jimbo la Uyole pamoja na Mbeya mjini kufanya maboresho katika sekta mbalimbali ikiwemo Miundombinu ya barabara ikiwemo barabara za mchepuko itakayoondoa magari makubwa kwenye barabara kuu (TANZAM) kwani Mkandarasi ameshalipwa fidia na serikali (48km) hivyo barabara hiyo ianze kujengwa kama inavyojengwa Barabara ya TANZAM.
Dkt. Tulia pia ameipongeza Mamlaka ya Maji mkoa wa Mbeya kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya Maji ingawa miradi hiyo haitoshelezi kulingana na idadi kubwa ya wananchi wa Mbeya na kusababisha adha kubwa kwa wananchi hao.
Dkt. Tulia ametoa salam Maalum kwa Waziri Mkuu, kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi mkubwa wa Maji wa Mto kiwira wenye zaidi ya Bilioni 117 ambao umeshaanza kutekelezwa na kuiomba Serikali pindi mkandarasi atakapopeleka cheti cha malipo aweze kulipwa na kumalizia mradi huo ili kusudi wananchi wa mkoa wa Mbeya kuweza kupona na shida ya Maji.
Dkt. Tulia amemaliza kwa kumuomba Waziri Mkuu, Halmashauri ya manispaa ya Uyole na kushukuru kwa eneo ambalo jengo la Halmashauri hiyo litajengwa na kwamba kazi imeshaanza kwa kuletewa Shilingi bilioni 1.
