Serikali ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa Meli kubwa na ya kisasa ya MV Mwanza iliyogharimu Bilioni 120 ikiwa na uwezo wa kubeba Tani 400 za mizigo na abiria 1,200 kwa wakati mmoja. Meli hii inatarajia kuanza safari zake rasmi katika Ziwa Victoria kuanzia Mwanza, Kagera na ukanda mzima wa Ziwa hivi karibuni.
Afisa Tarafa ya Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku Jana Ijumaa Disemba 19, 2025 ameshiriki Kikao cha pamoja kati ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) na wadau wa Bandari za Kagera, kikao kilichohusu kupokea na kutoa maoni ya wadau kuhusu nauli za meli hiyo mpya ya MV Mwanza. Kikao hiki muhimu cha wadau kimefanyika katika hoteli ya ELCT- Bukoba Mjini.
Kikao hicho kilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali (Mst) Hamis Maiga.
Kwenye Kikao hicho, Afisa Tarafa Bwanku ameshauri kuhakikisha meli hiyo kubwa ikianza safari zake rasmi muhimu iwe na route ya Bandari ya Kemondo kinyume na ilivyo sasa ambapo TASAC na TASHICO wanapendekeza meli hiyo ifanye safari zake kutoka Mwanza hadi Bukoba na isipite Kemondo huku akishauri pia nauli kupunguzwa ili wananchi wengi wafaidike na uwekezaji huo wa Serikali ya Tanzania.
