BIL 14.5 ZABADILISHA MAISHA; DARAJA LA NZALI LAANZA KUTUMIKA DODOMA


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameleta tabasamu kwa wananchi wa Nzali na Itiso baada ya kuanza kutumika kwa Daraja la Nzali lililogharimu Shilingi Bilioni 14.5 ambalo limekuwa ni suluhisho la changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwa miaka mingi, hususan wakati wa mvua.

Akizungumza katika hafla ya kuruhusu matumizi ya daraja hilo, Senyamule alisema kabla ya ujenzi wake wananchi walikumbwa na adha mbalimbali ikiwemo vifo vya watu na mifugo, kupotea kwa mali, wagonjwa kushindwa kufika hospitalini kwa wakati, watoto kukosa masomo na wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao.

Alisema Rais Samia, kwa kujali maisha na ustawi wa wananchi, aliamua kupeleka fedha hizo Nzali ili kuhakikisha wananchi wanapata daraja litakalowawezesha kufanya biashara, kupata huduma za afya kwa wakati na watoto kuhudhuria shule bila vikwazo

Aliongeza kuwa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 98 na daraja limeanza kutumika rasmi huku kazi ndogondogo zikiendelea.

Senyamule aliwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa daraja hilo kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kusafirisha mazao na kuendeleza biashara, sambamba na kuwa walinzi wa miundombinu hiyo, akisisitiza kuwa Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaoharibu au kuiba miundombinu hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, alisema ujenzi wa daraja hilo ulianza Novemba 15, 2024 na umehusisha daraja lenye urefu wa mita 60 na upana wa mita 11.4, makaravati manne pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita 1.5.

Aliongeza kuwa Daraja hilo limefikia asilimia 98 huku asilimia mbili zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba 30 mwaka huu.

Post a Comment

Previous Post Next Post