MAGEREZA MKOANI DODOMA WAPOKEA MAJIKO GESI NA MITUNGI YA KILO 15 KUTOKA REA


Watumishi wa Jeshi la Magereza mkoa wa Dodoma, tarehe 25 Novemba, 2025 wamepokea majiko ya gesi ya sahani mbili pamoja na mitungi yake ya kilo 15 zaidi ya 15,000 kutoka kwa Msambazaji; kampuni ya Lake Oil Tanzania ambapo ni uwezeshaji wa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kama sehemu ya jitihada ili kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akipokea majiko hayo pamoja na mitungi yake, kwa niaba ya Mkuu wa Gereza la Msalato mkoani Dodoma, Kaimu Mrakibu wa Gereza la Msalato; Tumaini Mgongo ameishukuru Serikali kwa kufikisha teknolojia za nishati safi ikiwemo majiko ya gesi ya sahani mbili pamoja na mitungi yake ya kilo 15 na kuongeza kuwa Askari na Watumishi wa Gereza la Msalato watayatumia na kuwa mabalozi wa nishati safi.

“Ninaahidi kwa niaba ya Watumishi wa Magereza kuwa, tutayatumia majiko haya na tutakuwa mabalozi kwa Wananchi wengi katika kutumia gesi kama chanzo cha nishati safi ya kupikia, majumbani mwetu” alisema Kamishna Mgongo.  

Kwa upande wake Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA; Dkt. Joseph Sambali amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Wananchi wakiwemo Watumishi wa Magereza ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024/2034 ambao unasisitiza angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

“Tukio la leo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na ni matumaini yetu kuwa baada ya Serikali kusambazia Magereza majiko haya pamoja na mitungi ya gesi, watafikiwa Jeshi la Magereza pamoja na Taasisi zingine” alisema Dkt. Sambali. 

REA kwa kushirikiana na Magereza wameendelea kuwafikia Watumishi wa Jeshi hilo ambapo, tarehe 25 Novemba, 2025 ilikuwa ni zamu ya Magereza mkoa wa Dodoma ambapo jumla ya majiko ya gesi ya sahani mbili na mitungi yake 15,068 imeanza kusambazwa mkoani humo ambapo usambazaji umezinduliwa rasmi katika Gereza la Msalato. 

Post a Comment

Previous Post Next Post