SERIKALI KUJENGA BARABARA YA LAMI IHUMWA–HOMBOLO


Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, amesema ujenzi wa barabara ya Ihumwa–Hombolo kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya Wakala wa Barabara (TANROADS) kukamilisha usanifu wa kina wa ujenzi wa barabara hiyo ambayo inagusa zaidi ya kata tatu za Jimbo la Mtumba.

Amesema barabara hiyo ni miongoni mwa miradi iliyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM na inalenga kurahisisha usafiri pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.

Akiendelea na kampeni zake katika Kijiji cha Mkoyo, Kata ya Hombolo Bwawani, Mavunde ameahidi pia kuwa atahakikisha anasogeza huduma  kupitia Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Tanzania(NIDA) ili kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri hadi mjini kufuata huduma hiyo muhimu.

Hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa vitambulisho.

Katika sekta ya elimu, Mavunde ameeleza kuwa Shule za Msingi na Sekondari HOMBOLO zimetemgewa fedha kwa ajili ya ukarabati  wa madarasa na matundu ya vyoo huku Shule Mpya ya Sekondari ya Anthony Mavunde itapanuliwa kwa kujengewa madarasa mawili mapya na maabara tatu za kisasa kupitia wadau wa maendeleo kutoka nchi ya Mauritius huku serikali ikiongeza darasa moja.

Amesema Tayari mkataba wa ujenzi umesainiwa na jumla ya shilingi milioni 242 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo, ambao unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa Hombolo na maeneo ya jirani.

Post a Comment

Previous Post Next Post