MIAKA 10 IMEKUWA YA MAPINDUZI MAKUBWA YA FIKRA NA UCHUMI RUFIJI -MHE.MCHENGERWA


Mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM)  wa Jimbo la Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema  akichaguliwa tena atashirikiana na wananchi wa jimbo hilo kuboresha uchumi baada ya mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika kipindi chake.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo wakati akinadi sera zake katika Mkutano Mkuu wa Wilaya wa kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena na  wanachama katika kata za Mbwara, Chumbi na  Mohoro.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema katika kipindi chote cha ubunge wake wa miaka 10  jimboni hapo  alibeba  fikra za wananchi wa Rufiji jambo ambalo limesaidia kutimiza ndoto za wananchi na maendeleo makubwa yanayoonekana.

Ameyataja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki kuwa ni pamoja na ujenzi wa  shule za kidato cha tano na sita kutoka shule moja hadi saba,  shule za kidato cha kwanza hadi nne zilikuwa nne tu na sasa zimefika 23.

Kuhusu Shule za Msingi amesema zilikuwa  20 na sasa zimefikia 63 huku  vituo vya afya vikiongezeka toka vitatu hadi tisa.

Pia amesema wakati anaanza ubunge jimbo halikuwa na barabara za ndani za lami lakini sasa lina takribani kilomita 20 na taa za barabarani zaidi ya 200.

"Ukweli ni kwamba Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa sana kwenye  jimbo letu. ni katika kipindi hiki ambapo tumeshuhudia  ongezeko la madaraja toka madaraja 3 hadi 7 ambapo daraja la Mohoro peke yake limegharimu bilioni 17". Amefafanua 

Akizungumzia mipango mahususi ya kiuchumi itakayosaidia  Mhe. Mchengerwa amesema tayari wamejitokeza wawekezaji wa Kilimo cha Migomba, miwa na kiwanda cha mafuta ya  mawese, na kusisitiza kuwa uwekezaji huu utazalisha ajira nyingi kwa akina mama na vijana.

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki Rufiji imepandishwa haji kuwa Halmashauri ya jiji jambo ambalo litawezesha kupata miradi mbalimbali ya Benki ya Dunia yenye thamani ya bilioni 30.

Pia amefafanua kwamba katika kipindi hiki jimbo  limeunganishwa umeme toka asilimia 17 hadi takribani asilimia  100 ya vijiji vyote vya jimbo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post