TUMEONGEZA IDADI YA WATALII KUFIKIA MILIONI 5.3 – WAZIRI CHANA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt.Pindi Chana (Mb) amesema chini ya uongozi imara wa Rais Samia, Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 5.3 na mapato yatokanayo na utalii kufikia dola za kimarekani bilioni 3.9.

Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alihutubia wananchi kwenye uwanja wa stendi ya zamani Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu leo Juni 18,2025.

Mhe. Chana ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kurekebisha kanuni za kifuta jasho/machozi.

"Mheshimiwa Rais nasimama kifua mbele kusema kwamba maelekezo yako yote tumetekeleza na hapa Bariadi tumepokea majina yasiyopungua 240 na wataalamu wako uwandani kulipa kifuta jasho/machozi katika vijiji vya Gilya, Senta, Nyamikoma, Salalia,Mwasilimbi,Matongo, Ng’alita, Mwandama,Mwantimba, Ihusi, Igabanyiro, Masewa na Mauchumu " amesema Mhe. Chana.

Sambamba na hilo Mhe. Chana amefafanua kuwa Serikali imeendelea kujenga vituo vya askari kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na kwa Bariadi vimejengwa katika maeneo ya Handajega, Duma na Ndabaka na vinaendelea kuongezwa.

Aidha amesema Serikali inatoa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa vijana (Village Game Scouts) kupitia chuo  cha Likuyu Sekamaganga kilicho chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

"Tumetoa mafunzo kwa askari wa vijiji (VGS) wasiopungua 390 kutoka vijiji takribani 13 vya Nyamikoma, Senta, Igabanilo, Mwatimba, Matongo, Salaliya, Mwauchumu, Chungu ,Damidami, Halawa, Ihusi, Mwasilimbi na Mwasinasi.

Mhe. Chana amesema Wizara inaendelea kufunga kola tembo viongozi ili kuweza kufuatilia mienendo yao, kuweka minara (observation tower) na kugawa vifaa mbalimbali vya kudhibiti tembo ikiwemo tochi, vuvuzela,filimbi, ndegenyuki na kugawa mabomu baridi katika vijiji mbalimbali ikiwemo Nyamikoma, Senta,Igabanilo, Mwantimba, Matongo,Salalia, Mwauchumu, CChungu,Damidami, Halawa, Ihusi, Mwasilimbi na Mwasinasi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia mapato ya retention ya asilimia 51 kubaki kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi na utalii.

Post a Comment

Previous Post Next Post