Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo, amekabidhiwa rasmi taasisi hiyo leo Juni 23, 2025 mbele ya Menejimenti ya Hospitali hiyo kutoka kwa aliyekuwa mtangulizi wake Prof. Mohamed Janabi aliyechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Dkt. Kimambo, ambaye awali alikuwa Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi Taasisi ya Tiba ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ameahidi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kutoa ushirikiano kwa viongozi na watumishi wote wa MNH.
"Nipo tayari kushirikiana na kila mmoja wenu kuhakikisha hospitali yetu inaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa Watanzania. Tutajenga juu ya mazuri yaliyowekwa tayari," amesema Dkt. Kimambo.
Kwa upande wake, Prof. Janabi ameishukuru menejimenti, wakurugenzi na watumishi wote wa MNH kwa ushirikiano waliompa kipindi cha uongozi wake. Amewataka kuendeleza mshikamano huo kwa kumpa ushirikiano Dkt. Kimambo ili hospitali iendelee kusonga mbele.
"Mafanikio yoyote hayapatikani kwa mtu mmoja. Ushirikiano wenu umekuwa msingi mkubwa wa hatua tulizofikia. Naomba mshikamano huo uendelee kwa mkurugenzi mpya," amesema Prof. Janabi.
Prof. Janabi aliteuliwa kuongoza MNH mwaka 2022, na anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake mapya WHO Julai 1, 2025 huko Brazzaville, Congo.