Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba, sheria, utumishi na utawala bora Zanzibar Bwana Mzee Ali Haji amesema kutekelezwa kwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Visiwani Zanzibar ni utekelezaji wa maono thabiti ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwataka wanaotekeleza kampeni hiyo kuhakikisha wanatafsiri vyema maono hayo kwa kuhakikisha haki inatendekea kwa kila mmoja anayestahili.
Mzee Ali amebainisha hayo Leo Jumatatu kwenye Viwanja vya Bustani ya Mwanamashungi Mkoa wa Kusini Pemba, wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo ya Kitaifa kwenye Mkoa wa nne Visiwani humo, uzinduzi uliofanywa na Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu Zanzibar Jaji Khamis Ramadhanil Abdallah.
Akizungumzia utekelezaji wa Kampeni hiyo visiwani Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu huyo amebainisha kuwa kufikia sasa Kampeni hiyo imeshatekelezwa katika Mikoa mitatu, wa nne ukiwa ni Kusini Pemba (ilipozinduliwa leo), akibainisha kuwa jumla ya wananchi 36, 788 wamefikiwa, kati yao wanaume wakiwa 16,992 na wanawake wakiwa 19,866, akiwapongeza wasimamizi na waratibu wa Kampeni hiyo kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kutafsiri dhamiri nje ya Rais Samia.
Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inatekelezwa nchi nzima ya Tanzania ambapo kwa Upande wa Tanzania bara imebakisha mkoa wa Dar Es salaam pekee ambapo kampeni hiyo itazinduliwa mwezi Juni mwaka huu ikienda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya Kampeni hiyo itakayozunguka tena kwenye Mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.