Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma Mhe. Mariam Ditopile, ameliambia Bunge kuwa kutokana na Mapinduzi makubwa ya sekta ya Kilimo pamoja na manufaa yaliyopatikana kwa wakulima ndani ya Miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Wakulima zaidi ya Milioni nane wa Tanzania wameahidi kumpa kura za kishindo kama ahsante ya tija kubwa iliyopatikana kwenye sekta hiyo.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/26, leo Jumatano Mei 21, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, Mhe. Mariam Ditopile amebainisha kuwa mafanikio hayo makubwa yanayoshuhudiwa kwa kipindi kifupi yametokana na utashi binafsi na imani ya Rais Samia kwenye sekta ya Kilimo.
"Wakulima wa nchi hii wanasema wanatambua kuwa tayari CCM imempitisha rasmi Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025,Kwa Tanzania nzima wapo zaidi ya Milioni 8 na tena wamesajiliwa, wanatambuana na wamejiandikisha kupigakura, Wanamuambia atoe shaka kura zote za wakulima ndani ya nchi hii zitaenda kwake na nia wanayo na sababu za kumuunga mkono wanazo." Amekaririwa Mhe. Ditopile.
Akizungumzia mafanikio ya Miaka minne ya Rais Samia ameeleza kwamba ruzuku zimekuwa zikitolewa kwenye Korosho, pamba na Tumbaku, ambapo kwa Tumbaku pekee jumla ya Bilioni 21 zimetolewa kwa wakulima, suala ambalo limesababisha Tanzania kuwa nafasi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku barani Afrika.
Ameeleza kwamba ni serikali ya Rais Dkt. Samia pia iliyoimarisha na kufufua ushirika nchini ambapo kwa mara ya kwanza pia ndani ya serikali ya Rais Samia, Ushirika umefanikiwa kuwa na Benki yake ya Taifa ya Ushirika iliyo na Makao yake Jijini Dodoma.
Aidha ongezeko la matumizi ya mbolea nchini limeongezeka kutoka tan 363,599 mwaka 2021/22 hadi tani 580, 628 mwaka 2022/23, ongezeko ambalo limetajwa kutokana na serikali kutoa mbolea ya ruzuku, kuimarisha uwezo wa kampuni ya mbolea (TFC) kwa kuipatia mtaji wa jumla ya Shilingi Bilioni 116.
Aidha Mhe. Ditopile pia ameeleza kuwepo kwa ongezeko kubwa la bajeti ya wizara ya kilimo ndani ya miaka minne ya Rais Samia, miradi mikubwa ya umwagiliaji pamoja uanzishwaji wa mashamba makubwa ya kilimo, suala ambalo amesema limesababisha sekta binafsi na sekta ya umma kujadili na kuingia kwa wingi kwenye kilimo nchini.
Ditopile anaungana na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ambaye wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo, mbali ya kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana, alieleza kwamba wakulima wa Tanzania ni miongoni mwa wapigakura muhimu na wa uhakika kwa Rais Samia, akieleza kwamba wanafikika kirahisi na wameunganishwa katika mtandao mmoja, wakifikia zaidi ya Milioni nane.