Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, leo amekutana na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na kueleza mafanikio makubwa ya sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya mada isemayo “Mafanikio ya Sekta ya Madini katika Kipindi cha Miaka Minne ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Katika hotuba yake, Waziri Mavunde alieleza kuwa bajeti ya Wizara imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 89 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi bilioni 231 mwaka 2024/2025, huku bilioni 224 zikiwa zimeidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Kiasi kikubwa kimeelekezwa katika ujenzi wa maabara za kisasa, ikiwa ni sehemu ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za maabara ya madini barani Afrika.
Aidha, sekta ya madini imeweza kufikia mchango wa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa (GDP) kufikia Desemba 2024, kabla ya lengo la 2025, hatua iliyotajwa kuwa ya kihistoria.
Waziri Mavunde alieleza pia kuhusu utekelezaji wa Mining Vision 2030 yenye kauli mbiu “Madini ni Maisha na Utajiri,” ikilenga kuongeza tafiti za madini kutoka asilimia 16 hadi 50. Sekta hiyo kwa sasa inachangia mzunguko wa fedha wa takriban trilioni 1.7, huku mauzo ya nje ya madini yakifikia asilimia 56.2 ya jumla ya mauzo ya nje ya nchi.
Kwa upande wa mapato, maduhuli ya sekta ya madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 162 mwaka 2015/2016 hadi kufikia bilioni 930 ndani ya mwaka huu wa fedha (2024/2025), huku lengo likiwa trilioni 1.
Kuhusu ununuzi wa dhahabu, Waziri alieleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza rasmi ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani, ikiwa ni utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2024. Katika miezi minane tangu kuanza kwa utaratibu huo, BoT imenunua tani 3.7 za dhahabu, hatua inayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri barani Afrika.
Serikali pia imechukua hatua kubwa kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo ya uchimbaji, kuwafutia leseni 2,648 zisizotumika, na kuwawezesha kwa mitaji na teknolojia kupitia STAMICO na benki za ndani. Vilevile, serikali imeanzisha vituo vya kukodisha mitambo kwa gharama nafuu ili kuongeza tija.
Katika kuongeza thamani ya madini, Waziri Mavunde alieleza kuwa eneo la mgodi wa zamani wa Buzwagi limegeuzwa kuwa eneo maalum la viwanda, likiwemo kiwanda cha kusafisha makinikia cha Tembo Nickel Refining Ltd.
Kwa upande wa madini ya vito, minada rasmi imerejeshwa, ikiwa ni juhudi za kuitangaza Tanzanite kimataifa kupitia minada iliyofanyika Mirerani na Arusha.
Sheria ya Madini imefanyiwa marekebisho ili kuhakikisha uchimbaji mdogo unafanywa na Watanzania pekee, huku wageni wakiruhusiwa kutoa msaada wa kitaalamu kwa masharti maalum. Marekebisho hayo pia yamepunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wawekezaji.
Waziri Mavunde pia alizungumzia miradi mikubwa kama ule wa Nyanzaga (Sengerema) unaoendelea kuvutia uwekezaji mkubwa, na kuipongeza STAMICO kwa kuongeza mapato yake kutoka bilioni 1 hadi bilioni 84 ndani ya miaka minne.
Kwa upande wa ajira, zaidi ya Watanzania 19,000 wameajiriwa moja kwa moja kwenye migodi, huku asilimia 97 wakiwa ni Watanzania. Pia, wapo wanaotoa huduma muhimu kama utengenezaji wa vifaa vya migodini.
Waziri pia alibainisha kuwa serikali iko mbioni kukamilisha mkakati wa kuendeleza madini mkakati kama graphite, nickel, na rare earths. Mpango maalum wa Mining for a Brighter Tomorrow tayari umeanza kuwasaidia wanawake na vijana kwa kuwapatia zaidi ya leseni 2,000 mkoani Mara.
Aidha, serikali iko kwenye mazungumzo ya kuanzisha sarafu ya dhahabu (Gold Coins) kwa ajili ya uwekezaji, pamoja na kuendelea na vikao vya majadiliano na wawekezaji ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Waziri Mavunde alihitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali imefanikiwa kuanzisha masoko 43 na vituo 109 vya ununuzi wa madini nchini, huku ushirikiano wa kimataifa ukiimarishwa kupitia mikataba ya ushirikiano na nchi mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza sekta ya madini nchini.