Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa rai kwa Watanzania wote kuwapuuza wanasiasa wanao washawishi kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Ndumbaro ametoa rai hiyo leo katika uwanja wa Mashujaa manispaa ya Bukoba wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Mkoani Kagera.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana kuwa ni Haki ya kila mtanzania mwenye vigezo kushiriki katika Uchaguzi.
"Katiba yetu iko wazi kabisa, vigezo ambavyo vitamzuia mtu kutoshiriki Uchaguzi ni endapo sio mtanzania, au ana matatizo ya akili, ni mhalifu aliyetiwa hatiani na ambaye hana kitambulisho cha mpigakura, sasa kama mtanzania hauna kasoro hizo kwanini usitumie haki yako kikatiba kushiriki uchaguzi ", amesisitiza Dkt Ndumbaro
Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa wapo wanasiasa ambao wamekuwa wakipotosha juu ya Haki za Binadamu wakijikita katika haki za kisiasa pekee wanasahau kumpongeza Mheshimiwa Rais anaayetekeleza haki kwa watanzania katika nyanja mbalimbali kama vile ujenzi wa miundombinu inayowezesha kuboresha maisha na kuleta maendeleo.
Aidha Dkt Ndumbaro ametoa wito kwa viongozi wa dini kukemea maovu hasa kwa wale wanaojichukulia Sheria mkononi na kugeuka chanzo cha migogoro pia familia zijikite katika kutafuta mapatano na sio kuongeza migogoro hususan ya ardhi na mirathi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa mkoa huo utawavua mamlaka wenyeviti wa vijiji na mitaa pamoja na kuwatengua watendaji wa mitaa na vijiji wanaosababisha migogoro ya ardhi kwani wao wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi mara kwa mara.
“Mkoa wa Kagera huu hata vitendo vya mauaji mara nyingi vinasababishwa na migogoro ya ardhi ,mara nyingi wenyeviti wa vijiji wanauza maeneo ya wananchi migogoro haiishi na hapohapo tunapata watu wanalipiza visasi ,sasa kama mkoa tunapanga kuchukua hatua madhubuti ,kuwawajibisha,” amesema Mwassa.
Mwassa ameongeza kuwa baada ya kuhitimisha kampeni hiyo mkoa umejipanga kuendeleza huduma za Msaada wa Kisheria kwa wananchi kwakuwa watakuwa wamepata uzoefu kupitia watalaamu wanaoshiriki katika utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika halmashauri zote za mkoa huo.
