RAIS SAMIA NI CHACHU YA MAENDELEO YA MALIASILI NA UTALII". MHE. CHANA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta mchechemko mkubwa wa maendeleo makubwa katika sekta ya Maliasili na Utalii hali inayopelekea hari kubwa  ya uchapaji kazi kwa watumishi wa Wizara hiyo. 

Ameyasema hayo Jijini Dodoma leo tarehe 17 Aprili 2025 wakati wa ufunguzi  wa Mkutano wa 33 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Maliasili na Utalii. 

Amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kuongeza mapato ya Sekta na kufikia Dola Bilioni 3.9 sambamba na idadi ya Watalii kufikia milioni 5.3 ambapo imevuka lengo la watalii milioni 5 ifikapo 2025.

Ameongeza kuwa mafanikio mengine ya Sekta hiyo ni kuongezeka kwa mchango katika Pato la Taifa  (GDP) ambapo ni asilimia 21%, mchango wa Fedha za kigeni asilimia  30.9% (utalii ikiwa 25%  na Misitu na Nyuki 5.9%  na kuifanya wizara hiyo kuwa namba moja nchini kwa kuleta fedha za kigeni. 

“Tanzania imetwaa Tuzo saba (7) za utalii ikiwemo Eneo linaloongoza kwa Utalii wa Safari Duniani (world’s Leading Destination),  Eneo Linalovutia zaidi Kiutalii Afriak (Africa’s Leading Destination 2024), Tuzo ya kivutio bora cha Utalii (Afican Leading Tourism Attraction 2024)“ Mhe. Chana amesisitiza.

Aidha, Mhe. Chana licha ya kuwapongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya, amewaelekeza kuendelea kuongeza na kukuza wigo wa bidhaa/mazao ya utalii na kuongeza mapato kutoka Dola za Marekani 2.6 Bil mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Kimarekani 6 Bil mwaka 2025. 

“ Mojawapo ya njia za kufikia malengo haya ni kuimarisha utalii wa uwindaji wa wanyamapori, kukuza utalii wa mikutano na kuendeleza utalii wa fukwe, kuimarisha ukusanyaji mapato, n.k. 

Vilevile Mhe. Chana ameelekeza Watendaji na Watumishi kuendelea kuimarisha usimamizi, ulinzi na uhifadhi wa maliasili kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho kwa kuendelea kujengae uwezo wa wadau katika kusimamia rasilimali za wanyamapori, misitu na nyuki, kudhibiti ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu na nyuki, kuhamasisha wananchi kuanzisha ranchi, mashamba na bustani za wanyamapori, kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji katika sekta.

Awali akitoa neno la utangulizi, Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, CP. Benedict Wakulyamba amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuzingatia ustawi watumishi na maslahi yao kwa lengo la kuikuza Sekta hii kwa maslahi mapana ya Taifa.

"Tutaendelea kuzingatia ustawi wa rasilimaliwatu, mafunzo kwa watumishi na ushiriki wao katika shughuli za Kitaifa" amesema CP. Wakulyamba.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Utalii), Nkoba Mabula, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, K atibu wa Baraza,Viongozi wa TUGHE- Taifa na Mkoa, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) Tawi la Wizara, Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wakuu wa Idara/Vitengo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Post a Comment

Previous Post Next Post