Waziri wa Madini Mh Anthony Mavunde leo asubuhi amefanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Marvel Gold Ndg. Timothy Strong juu ya uwekezaji wa kampuni hiyo kwenye sekta ya madini.
Kampuni hiyo kutoka nchini Australia imefika kujitambulisha na kuelezea mpango wao wa kuanzisha mgodi mkubwa wa dhahabu katika Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara.
“Tumeichagua Tanzania kwasababu ni nchi ambayo ina amani na usalama na mazingira mazuri ya uwekezaji,na tumevutiwa na mpango mzuri wa Rais Dkt. Samia S. Hassan kuvutia uwekezaji nchini Tanzania.
Tutafanya utafiti wa kina kwa kurusha ndege na baadaye kukamilisha hatua zote za utafiti wa madini.
Tunategemea kuanza zoezi la utafiti wa kina ifikapo mwezi Septemba 2025”Alisema Strong
Awali Waziri Mavunde aliwapongeza wadau hao kwa kuichagua Tanzania kufanya uwekezaji wao na kuwahakikishia kwamba serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha miradi kama hiyo yenye dhamira ya kukuza sekta ya madini inafanikiwa.
“Ninapokea watu wengi sana wenye nia kama ya kwenu,asilimia kubwa si wakweli kutekeleza mipango yao na wamekuwa na maneno mengi kuliko vitendo
Ni imani yangu kwamba Kampuni hii itafanya kazi kubwa ya utafiti ili kama nchi tufanikiwe kupata mradi mwingine mkubwa wa uchimbaji madini ya dhahabu Mkoani Manyara”Alisema Mavunde