Waziri wa Ujenzi Mh. Abdallah Ulega amewahakikishia wananchi wa kata ya Ntyuka kukamilika kwa barabara ya Ntyuka-Mvumi-Kikombo ambayo ujenzi wake hivi karibuni ulisimama.
Waziri Ulega ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 inayojengwa kwa awamu mbili na wakandarasi wawill ambao ni CHICO pamoja na China First.
Aidha, Ulega amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais Samia ni kuhakikisha kuwa miradi yote ya Sekta ya Ujenzi iliyosimama inaendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa na tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
"Mmeona katika muda wa hii miezi mwili, Rais Samia tayari amelipa malipo ya wakandarasi ya takribani shilingi bilioni 254, matumaini yetu tunataka kuona kazi zikiendelea," amesema Ulega.
Kadhalika, Ulega amemhakikishia Mkandarasi CHICO kuwa atalipwa malipo anayodai katika barabara hiyo na hivyo kumtaka arudi eneo la ujenzi na kuendelea na kazi usiku na mchana ili ikamilike kwa wakati na wananchi kuweza kunufaika na fursa ya uwepo wa barabara hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Mh. Anthony Mavunde amesema kuwa barabara ya Ntyuka - Mvumi- Kikombo ni barabara ya kihistoria ambapo serikali chini ya Rais Samia imefanya kazi kubwa kuifikisha mpaka hapo ilipofika na kuiomba Serikali kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni mkombozi kutokana na uwepo wa hospitali kubwa ya macho iliyopo eneo la Mvumi na hospitali ya DCMC inayotoa huduma nchi nzima na pia kuunganisha maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.