Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation Bi. Doris Mollel amebainisha kuwa sababu kubwa iliyomfanya kuanzisha vuguvugu la kutaka mabadiliko ya sheria ya mwaka 2024 kwa Wazazi wanaopata watoto njiti ni kutokana na changamoto nyingi walizokuwa wanakutana nazo Wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto hao ikiwemo matatizo ya kiafya, msongo wa mawazo na kufutwa kazi kutokana na kutumia muda mrefu Hospitalini.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya Bunge na Serikali kupitisha mabadiliko ya sheria hiyo Januari 31, 2025, Doris ameeleza kuwa tangu mwaka 2017 wamekuwa na shughuli, vikao na harakati mbalimbali za kupambania mabadiliko hayo, Wazo likianza mwanzoni mwa mwaka 2017 wakati alipotembelea wodi ya watoto njiti kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, alipoenda kuchangia vifaa tiba mbalimbali Hospitalini hapo.
Doris amesema miongoni mwa shughuli zilizofanyika mwanzoni mwa vuguvugu hilo ni pamoja na vikao zaidi ya 50 vikihusisha watu mbalimbali ikiwemo Umoja wa Wake wa Viongozi Nchini (Millenium Group), Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG), Wanasheria wa Wizara mbalimbali, Mawaziri, Wabunge wanawake, Wafanyakazi wanawake, Chama cha Madaktari wa Watoto wachanga pamoja na Kamati mbalimbali za kudumu za bunge na Maafisa wa Wizara mbalimbali serikalini.
Mwaka 2021, Taasisi ya Doris Mollel Foundation ikaanzisha Ajenda ya "Mtoto njiti" ambapo baadae 2023, Chama cha Wafanyakazi wa serikali na Afya Tanzania (TUGHE) na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) nao waliunga mkono jitihada hizo za Doris Mollel Foundation, suala ambalo lilipelekea mwaka 2024 wakati wa sherehe za siku ya Wafanyakazi duniani, Rais Samia Suluhu Hassan kutoa kauli yake ya kwanza hadharani, kupitia kwa Makamu wake wa Rais, akitangaza ujio wa marekebisho ya Sheria hiyo ya Kazi.
Akimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Sheria hiyo pamoja na aliyekuwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri Angellah Kairuki, Doris Mollel amesema kupitia marekebisho hayo ya sheria, Tanzania sasa inakuwa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zimetengeneza mazingira Jumuishi, bora ya kazi na yenye kuzingatia afya ya Wazazi wanaopata watoto njiti kote Tanzania.
Wakati wa Kikao cha Bunge Mjini Dodoma Januari 31, 2025, Serikali kupitia kwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, ajira na wenye ulemavu Mhe. Ridhiwan Kikwete, Serikali ilitangaza kuwa kuanzia sasa Mfanyakazi mwanamke atakayejifungua mtoto njiti likizo yake itaanza kuhesabiwa baada ya kufikisha wiki 40 za ujauzito na baba wa mtoto njiti atakayezaliwa, atapewa siku saba za mapumziko na hii ni kufuatia marekebisho ya sheria ya kazi ya mwaka 2024.