Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) na Baraza la Uhandisi la India (ECI) wameanza utekelezaji wa makubaliano kati yao ambayo yalisainiwa mwezi Disemba 2024 lengo kuu likiwa ni kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo.
Hayo yameelezwa na Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Eng. Bernard Kavishe katika Semina ya 18 ya uelekezi kwa wahitimu 362 wa uhandisi waliopo katika Mpango wa Mafunzo kwa vitendo kwa Wahandisi Wahitimu (SEAP) inayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.
Eng. Kavishe ameeleza kuwa makubaliano hayo yameandaa dira kuelekea mkataba wa kushabihisha viwango na kutambua tuzo zinazotolewa na pande zote mbili (MRA), ambao utarahisisha kubadilishana wataalam kati ya Tanzania na India.
Ameongeza kuwa India ilianza kufundishwa uhandisi na Waingereza hivyo kuna nafasi kubwa ya kujifunza zaidi kwao.
Kuhusu Semina hiyo, Eng. Kavishe ameeleza kuwa inalenga kuwapatia wahitimu wapya ujuzi, maarifa, na mtazamo sahihi ili kuendeleza taaluma yao ya uhandisi.
Eng. Kavishe ametaja mada mbalimbali zitakazojadiliwa katika Semina hiyo ikiwa ni pamoja na Muhtasari wa Mpango wa SEAP, Maadili ya Uhandisi na Kanuni za Mwenendo, Sheria ya Usajili wa Wahandisi, Kanuni na taratibu za usajili, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa wa ERB, Uadilifu katika Uhandisi na Afya na ustawi wa wahandisi.
Akizungumza wakati akifungua Semina hiyo, Katibu wa ECI Dk. Priya Ranjan Swarup ameeleza kuwa ECI na ERB zina mlengo mmoja hivyo ushirikiano huo utakuwa na tija kwa Tanzania na India.
Ameeleza kuwa ECI ni chombo kikuu cha kusimamia taaluma ya uhandisi nchini India, kikiwa na jukumu la kudumisha viwango vya juu vya umahiri wa kitaaluma.
Mhandisi Asha Mahimbo ni mmoja wa washiriki wa semina hiyo anasema, SEAP ni msaada mkubwa kwao kwani itawasaidia kupata uzoefu na hivyo kuwapa unafuu wa kupata ajira mapema kwa kuwa inawasaidia kujua soko la ndani na nje linahitaji wahandisi wa aina gani.
Aidha, katika Semina hiyo jumla ya wahandisi 236 wamekula kiapo cha utii cha Uhandisi na takribani Wahandisi Wahitimu 362 wamehudhuria mafunzo hayo na wengine wameshiriki kwa njia ya mtandao.
Ujumbe wa Baraza la Uhandisi la India (ECI) ukiongozwa na Dkt. Priya Ranjan Swarup, ambaye ni Katibu wa ECI upo nchini Tanzania kwa siku sita (6).