CHANGAMOTO ZIFANYENI KUWA FURSA KATIKA HUDUMA ZA AFYA ZA UBINGWA NA UBINGWA BOBEZI


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi kuongeza ubunifu katika utolewaji wa huduma bora za afya ikiwemo huduma za ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuzifanya changamoto zilizopo kuwa fursa katika hospitali hiyo. 

Waziri Mhagama ametoa maelekezo hayo leo Februali 18, 2025 Mkoani Pwani baada ya kuzindua bodi hiyo mpya ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Pwani, Tumbi inayosimamiwa na kuongozwa na Mwenyekiti wake Bi. Zalia Kawawa Mbeo yenye wajumbe tisa(9). 

"Hakikisheni mnafuatilia masuala yote yanayohusu hospitali yetu ya Rufaa ya Tumbi pamoja na kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambao ni zaidi ya Shilingi Tilioni 6.7 zimewekezwa katika Sekta ya Afya, pamoja na kununua magari ya wagonjwa na kuyaleta hapa ili iwasaidie kukamisha mipango yenu vizuri," amesema Waziri Mhagama. 

Pia, Waziri Mhagama ameitaka Bodi hiyo kulinda na kusimamia rasilimali watu ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kukutana na watumishi wa hospitali hiyo kwa kuzungumza nao ili kama wanachamgamoto waweze kuzigeuza kuwa fursa kwao. 

"Agizo langu jingine kwa bodi, simamieni vizuri rasilimali watu ni rasilimali muhimu kwakuwa kama huna watu wa kufanya kazi huwezi kufanikiwa, ukiwa na fedha kama huna rasilimali watu wanaoweza kusimamia fedha huwezi kufanikiwa," amesema Waziri Mhagama. 

Aidha, Waziri Mhagama amesema Sera ya Afya ya mwaka 2007, kipengere cha 8.2 imeelekeza kuwepo kwa vyombo vya kisheria, ikiwa ni pamoja na uwepo wa bodi katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa na zitateuliwa bodi hizo na mamlaka husika. 

"Kwa hiyo ninawakumbusha bodi kuwa mpo hapa kisheria na mnafanya kazi kisheria, msiogope, tekelezini majukumi yenu kwa kuzingatiaa sheria na taratibu zilizopo, lakini msitishe watu kwa kukiuka sheria na taratibu zilizopo," amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali itaendeleza juhudi za kuimarisha Sekta ya Afya kwa ujumla wake ikiwemo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi ili kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wanachi. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi mpya ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Pwani- Tumbi, Bi. Zalia Kawawa Mbeo ameahidi kusimamia na kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Mhe. Waziri Mhagama ikiwemo kusimamia  ubora wa huduma za afya za kibingwa katika Hospitali hiyo. 

"Mhe. Waziri wa Afya, mimi pamoja na wenzangu tunakuahidi tutatumia juhudi, weledi, utaalamu, uzalendo na kila tunaloweza kufanya katika kuhakikisha tunatoa usimamizi wa huduma za afya kupitia hospitali yetu ya Tumbi, lengo  likiwa ni kuboresha huduma za afya," amesema Bi.  Mbeo

Post a Comment

Previous Post Next Post