Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Semesi, amesema kuwa ongezeko la majanga kama mafuriko na maporomoko ya ardhi limechangiwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira. Ameyataja baadhi ya maeneo yaliyoathirika kuwa ni Katesh katika Wilaya ya Hanang (Manyara), Kawetere (Mbeya), na Mamba Miamba (Same, Kilimanjaro).
Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizotolewa Januari 23, 2025, zinaonyesha kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara, Arusha, Kilimanjaro, na Manyara, huku Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, na Shinyanga zikitarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Mvua hizi zimekuwa zikiathiri makazi ya wananchi, kusababisha uharibifu wa mashamba, upotevu wa mali, na hata vifo. Sekta za kilimo, mifugo, na maji zimeathirika kwa kiasi kikubwa, hali inayoweza kuhatarisha upatikanaji wa chakula na ubora wa maji. Miundombinu muhimu kama barabara, umeme, na mawasiliano pia imeharibika, hali inayoleta changamoto kubwa kwa wananchi. Uchafuzi wa vyanzo vya maji umesababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa za matumbo, jambo linalohitaji tahadhari za haraka.
Kutokana na hali hii, NEMC inatoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa kutoka TMA na kuchukua tahadhari za mapema. Wananchi wanashauriwa kuepuka kuishi katika maeneo hatarishi kama mabonde na kandokando ya milima ili kuepukana na athari za maporomoko ya ardhi na mafuriko. Pia wanakumbushwa kuhakikisha mifereji ya maji inasafishwa na taka ngumu hazitupwi kiholela ili kuzuia kuziba kwa mifumo ya majitaka na maji ya mvua.
Aidha, Mkurugenzi wa NEMC amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kufuatilia kwa karibu maeneo ya uchimbaji wa madini na vifusi ili kuhakikisha usalama wa jamii husika. Wasimamizi wa vyombo vya usafiri wametakiwa kuwa makini wanaposafiri, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa. Wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa viongozi wa maeneo yao kuhusu athari za mazingira zinazoweza kujitokeza ili hatua za haraka zichukuliwe.
Kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, wananchi wanakumbushwa kuepuka ujenzi kwenye maeneo hatarishi kama kandokando ya mito, mabonde, fukwe za bahari, na ardhi oevu. NEMC imesisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuchukua hatua za kujilinda na kulinda mazingira, kwani mazingira ni uhai wetu na ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha yanahifadhiwa kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.