ZAIDI YA WATU MILIONI 5 WAPATIWA KINGATIBA DHIDI YA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Afya, imeadhimisha Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani (World NTD Day) kwa kutoa huduma mbalimbali za kinga na matibabu kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amesema maadhimisho haya ni sehemu ya jitihada za Serikali na wadau wa sekta ya afya kuhakikisha magonjwa haya yanatokomezwa nchini.

"Siku hii ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa kwa umma kuhusu magonjwa haya na hatua zinazochukuliwa kuyatokomeza. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tuungane. Tuchukue Hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele’," alisema Waziri Mhagama.

Ameeleza kuwa Tanzania imekuwa mshiriki wa maadhimisho haya tangu yalipoanzishwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2021. Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imefanikiwa kudhibiti magonjwa kama matende, mabusha, trakoma (vikope), usubi, kichocho, na minyoo ya tumbo.

Katika kipindi cha mwaka 2024, zaidi ya watu milioni tano walipatiwa kingatiba dhidi ya magonjwa haya, huku Serikali ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 38 katika utoaji wa dawa, vifaa tiba, na huduma za kinga.

Waziri Mhagama ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni za kingatiba kwa kuhakikisha wanajitokeza kupata matibabu, kuzingatia usafi wa mazingira, na kutumia vyoo bora ili kupunguza maambukizi ya magonjwa haya.

Maadhimisho ya mwaka huu yamehusisha utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu bure kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kambi maalum ya afya iliyofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba, Mtwara

Post a Comment

Previous Post Next Post