Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya huduma za dharura kwa kuiwekea Mifumo ya mawasiliano ya kidigitali katika hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali zingine nchini ili kuwa rafiki na wezeshi zaidi kwa wahitaji na watumiaji na kufikia lengo la kuokoa maisha.
Dkt. Jingu amesema hayo Januari 9, 2025 Jijini Dar es Salaam katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati alipotembelea Mradi wa kuimarisha huduma za matibabu ya dharura ambapo amesema huduma za dharura ni eneo muhimu sana kwa ustawi wa jamii katika kuokoa maisha pale zinapotokea changamoto zenye madhara kama ajali, ugonjwa wa ghafla na nyinginezo.
“Huduma za Dharura haziishi kwenye Ambulace tu, bali tunataka mtu anayepata dharura ya ajali au ugonjwa wa ghafla aweze kuhudumiwa vizuri na kwa haraka kwani kwa sasa mfumo wa mawasiliano unahitaji kuwa bora na kuimarika, ili kuimarisha mfumo wa matibabu wa huduma za Dharura,” amesema Dkt. Jingu.
Amesisitiza Serikali ikiendelea na uboreshaji huo ni vyema wanaohusika kuhakikisha vifaa vyote vya dharura ikiwemo vifaa tiba na magari ya kubebea wagonjwa wa dharura vinatumika ipasavyo kama ilivyoelekezwa na Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa mapokezi ya magari ya wagonjwa mapema Mwaka 2024.
“Wengi Mtakuwa mnafahamu kama tumenunua magari ya dharura mengi, sasa haya magari tuyaratibu ili yafanye kazi iliyokusudiwa na Mhe. Rais alielekeza kwamba vifaa vyote vya dharura yakiwemo magari haya yatumike ipasavyo na ili kufanya kazi vizuri tunahitaji pia mfumo wa mawasilino wa kufuatilia haya magari pamoja na vifaa vingine yanafanya kazi wapi, namna gani uimarishwe,” amesema Dkt. Jingu.
Katika hatua nyingie, Dkt. Jingu ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na jinsi ilivyojipanga kila siku kupokea dharura kutoka hospitali mbalimbali nchini, watu binafsi na wale wanaoletwa na Jeshi la Polisi na kupata huduma kupitia Idara ya Tiba na Magonjwa ya Dharura pamoja na Kitengo cha Dharura kwa kina mama wajawazito.