LEGURUKI KUWA KITUO CHA AFYA MWAKA WA FEDHA 2025/26



Zahanati ya Kijiji cha Leguruki, iliyopo Kata ya King'ori katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, itabadilishwa kuwa kituo cha afya ifikapo mwaka wa fedha 2025/26, hatua inayolenga kuwahudumia wananchi zaidi ya 20,000 ambao kwa sasa wanasafiri umbali wa zaidi ya kilomita 44 kufuata huduma za afya.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amebainisha mpango huo wakati wa ziara yake kijijini Leguruki leo Januari 09, 2025 akisisitiza umuhimu wa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo.

 Amesema kuwa uwepo wa kituo cha afya utakuwa mkombozi kwa wananchi hao na kuitaka halmashauri kuweka suala hilo katika mpango kazi wa mwaka wa fedha 2025/26.

Dkt. Mollel ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha sekta ya afya ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora karibu na makazi yake. "Wananchi wa Leguruki wana kila sababu ya kujengewa kituo cha afya ili kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya matibabu," amesema Dkt. Mollel.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Bw. Amiri Mkalipa, ameeleza kuwa kata hivyo inahitaji kituo cha afya pamoja na mahitaji ya miundombinu muhimu, ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la mama na mtoto, bohari ya dawa, wodi za wagonjwa, na jengo la mionzi.

Bw. Mkalipa amemuomba Dkt. Mollel kusaidia kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa haraka, akibainisha kuwa gharama za kufuata huduma maeneo ya mbali ni kubwa kwa wananchi.

Kituo cha afya cha Leguruki kinatarajiwa kuwanufaisha wakazi wapatao 21,256 kwa kuwapa huduma za afya karibu na makazi yao. Hii itapunguza gharama na umbali wa kutembea kwa ajili ya matibabu, hivyo kuongeza urahisi wa kupata huduma na kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa eneo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post