MIREMBE YATOA TATHIMINI YA UTOAJI HUDUMA MWAKA 2024



Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imesema kuwa zaidi ya asilimia 34 ya watanzania kwa mwaka 2024 wameongezeka na kupatiwa matibabu ya afya ya akili ukilinganisha na mwaka 2023.r

Hayo yamebainishwa leo Januari 10, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Mahusiano ya Umma kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Christian Elias Alais kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt. Paul Lawala wakati akitoa tathmini ya hali ya utoaji Huduma kwa mwaka 2024.

Amesema ongezeko hilo ni ishara tosha kuwa jamii sasa inapata uelewa juu ya umuhimu wa magonjwa ya akili ndio maana watu wengi wanajitokeza kupata matibabu ya magonjwa ya akili kutokana na kazi kubwa inayofanywa na hospitali hiyo ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya magonjwa ya akili, afya ya akili na changamoto za afya ya akili. 

"Mwaka jana tuliongeza wigo wetu wa utoaji elimu ya afya ya akili kwenye jamii na tumeona matokeo yake, hii inaonesha jamii ilituelewa vizuri na kuchukua hatua ya kupata matibabu sahihi ya afya ya akili kutoka kwetu" amesema  Alais 

Alais amesisitiza jamii kuendelea kujitokeza kupata elimu ya afya ya akili ili kusaidia wananchi kupata matibabu sahihi kwa wakati na kupunguza tatizo la magonjwa ya akili katika taifa.

Vile vile Alais ameeleza kuwa katika eneo la Saikolojia wananchi pia wamejitokeza kwa wingi kupata ushauri ambapo zaidi ya watu 500 kwa mwaka 2024 wamepata kuhudumiwa ukilinganisha na mwaka 2023 walihudumia watu  ya 200 katika eneo la Saikolijia sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 75 ukilinganisha miaka hii miwili. 

Aidha amesema kuwa kwa mwaka 2024 wamehudumia wagonjwa zaidi ya 52,000 kwa magonjwa yote ukilinganisha na mwaka 2023 walihudumia wagonjwa  49,000 ambayo ni ongezeko la asilimia tano.

Hata hivyo amewakaribisha wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata Huduma mbalimbali kwa mwaka 2025 ambapo wamejipanga kutoa Huduma bora katika ubingwa na bingwa bobezi ya magonjwa ya akili, Huduma za kibingwa za mwili na afya ya akili kwa watoto na vijana pamoja na tiba za kisaikoloijia.

Post a Comment

Previous Post Next Post