FANYENI KAZI KWA HARAKA KUENDANA NA KASI YA MAENDELEO - MHAGAMA



Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka bodi mpya ya Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ambukizi Kibong'oto kufanya kazi kwa haraka ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sekta ya afya katika kuwahudumia wananchi. 

Waziri Mhagama amesema hayo leo Januari 10, 2025 baada ya kuzindua Bodi  mpya  ya Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ambukizi Kibong'oto ikiongozwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo Prof. Muhammad Bakari Kambi.

"Niitake bodi hii mpya, kufanya kazi kwa haraka ili kuendana na kasi ya maendeleo yanayoletwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta yetu ya afya, tunaweza kufanya kazi ya miaka 10 ndani ya miaka mitatu, hii inawezekana, mfano Serikali kuhamia Dodoma ilikuwa ni mipango ya miaka 30 nyuma lakini imefanyika ndani ya miaka kama sita hivi," amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama ameielekeza Bodi hiyo kusimamia utolewaji wa huduma bora za tiba na kinga dhidi ya magonjwa ambukizi, kufanya tafiti za kisayansi za tiba ya binadamu, mafunzo, ubunifu na ushauri pamoja na kutoa huduma bora za afya ya jamii na ufuatiliaji wa vimelea vya magonjwa ya kuambukiza.

"Naishukuru sana bodi iliyopita kwa kufanya kazi kubwa lakini nina imani kubwa na bodi hii mpya kuwa itaenda kuleta mabadiliko makubwa katika hospitali yetu na lengo kubwa ni kuwahudumia wananchi kwa kupata huduma bora na kwa wakati," amesema Waziri Mhagama.

 Aidha amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuibeba sekta ya afya na Wizara itahakikisha inatoa huduma za afya kwa ubora huku ikiendelea kuchukua uzofu kwa mataifa mengine ambako inaendelea kupeleka wataalam  kwenda kusoma nje katika fani mbalimbali za ubingwa na ubingwa bobezi. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Bw. Ismail Rumatila akimuwakilisha Katibu Mkuu Dkt. John Jingu ameihakikishia Bodi hiyo mpya kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na hospitali ya Kibong’oto katika kutatua changamoto zilizopo ikiwemo mchakato wa kuboresha maslahi ya watumishi. 

"Lakini pia tutaendelea kuimarisha miundombinu, kuongeza vifaa vya kisasa pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali watu na fedha  unapewa kipaumbele cha juu ili wananchi waendelee kupata huduma bora," amesema Bw. Rumatila

Nae, Mwenyekiti wa Bodi hiyo mpya Prof. Muhammad Bakari Kambi amemuahidi Waziri wa Afya kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa ikiwemo kufanya kazi kwa kasi ili kuendana na kasi ya maendeleo katika sekta ya afya.

Post a Comment

Previous Post Next Post