Serikali imewataka wananchi kuunga mkono agenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuwasaidia Watoto waliozaliwa kabla ya wakati pamoja na huduma za mama na mtoto ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.
Wito huu umetolewa leo Agosti 17, 2024, na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa matembezi ya amani yaliyoandaliwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto, pamoja na watoto waliozaliwa kabla ya wakati (Njiti).
Dkt. Mollel amesisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi, kwa kuwa afya ni rasilimali muhimu kwa maisha ya mwanadamu.
“Rais wetu amefanya kazi kubwa ya kuwekeza fedha, rasilimali watu, vifaa tiba na teknolojia ili kupunguza vifo vitokanavyo na mama na mtoto ambapo mpaka sasa kazi kubwa imefanyika na kupunguza vifo hivyo”. Amesema Dkt. Mollel
Aidha, Dkt. Mollel amebainisha kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imepiga hatua kubwa ya kufikia malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya kupunguza vifo vitokanavyo na mama na mtoto ikiwa ni miaka miwili kabla ya mwaka uliopangwa wa 2025.
Dkt. Molell ameongeza kuwa ni muhimu kwa jamii kuendelea kuunga mkono agenda ya Rais Samia ya kuboresha sekta ya afya kwa kushiriki kikamilifu kwenye juhudi za serikali kwa kufanya hivyo, jamii itachangia katika kufanikisha malengo ya kuboresha huduma za afya na kuhakikisha ustawi wa wananchi wote.