Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua kituo cha kupokea na kupoza umeme katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) chenye uwezo wa megawati 34 ambacho sasa kinawezesha GGML kuanza kutumia umeme wa gridi kwa matumizi yake badala ya mafuta na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.
Baada ya kuzindua kituo hicho tarehe 13 Agosti 2024 wilayani Geita mkoani Geita, Dkt.Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho ni alama halisi ya umoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Sekta Binafsi kwani mradi huo umehusisha ujenzi wa laini ya umeme ya kV 33 ambayo imejengwa na TANESCO kwa gharama ya shilingi bilioni 8.04 huku GGML ikijenga kituo cha kupoza umeme kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 24.
Amesema GGM ilikuwa inatumia shilingi bilioni 130 kwa mwezi kama gharama za uendeshaji na kwenye umeme wa mafuta ilikuwa inatumia shilingi bilioni 13.4 kila mwezi na kuathiri mapato yake kwa Serikali, hivyo kuanza kazi kwa kituo hicho kunapunguza gharama za uendeshaji kwa mgodi na kupelekea Serikali kuongeza mapato yake, kuongeza ajira na pia GGM kuweza kutanua shughuli zake.
Dkt.Biteko ameipongeza kampuni hiyo kwa kuanza kutumia umeme wa gridi ambao unapunguza gharama za uendeshaji ambapo ametoa angalizo kuwa, kupungua kwa gharama hizo kuguse pia watumishi kwa kuboresha maslahi yao.
Ameeleza kuwa, umeme mwingi unaozalishwa kwa sasa unatoa uhakika wa kwenda kwa wananchi na walaji wakubwa kama GGM na kuweka mkazo kuwa, hayo ni matokeo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuijali sekta binafsi.
Kuhusu usambazaji umeme mkoani Geita amesema kuwa Mkoa una Vijiji 486 na kati ya hivyo vijiji 483 vina umeme sawa na asilimia 99.38.
Ameongeza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vitongojini mkoani Geita inaendelea ambapo kati ya vitongoji 2,197, vitongoji takriban 1000 tayari vina umeme.
Wabunge mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Rais Samia pamoja na uongozi wa Wizara ya Nishati kwa kutekeleza mradi huo ambao una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi na mgodi wenyewe.
Makamu wa Rais wa kampuni ya Anglo Gold Ashanti-Tanzania anayeshughulikia Miradi Endelevu, Simon Shayo ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na miundombinu madhubuti ya umeme inayowawezesha kufanya biashara kwa ufanisi na kusema mradi huo kwa GGM unawawezesha kupata umeme wa gridi na kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta ambapo gharama zitapungua kwa asilimia 92.