Naibu Waziri, Wizara ya Nishati, Mhe. Judith Kapinga, leo tarehe 16 Agosti, 2024 ameweka historia kwa kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kijiji cha Mpingi, Kata ya Matimila, Halmashauri ya wilayani Songea mkoani Ruvuma, ambapo vijiji ambavyo havijaunganishwa na umeme ni viwili (2) tu kati ya vijiji 554, sawa na asilimia 99.4.
Naibu Waziri Kapinga, ameongoza zoezi hilo, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Mzunguko wa Tatu (Awamu ya Pili) katika wilaya hiyo pamoja na kuzungumza na Wananchi katika kijiji cha Mpingi.
Akizungumzia Miradi ya kusambaza nishati ya umeme vijijini, Mhe. Kapinga amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini, lengo ni kuinua maisha ya Watu ambapo msisitizo ni kufikisha umeme kwenye vituo vya afya, taasisi za elimu, taasisi za dini, masoko, visima vya maji na mashambani na kuongeza kuwa kwa Watanzania umeme sasa siyo starehe bali ni hitaji la muhimu.
“Niwatoe hofu kuwa Wananchi ambao hamjafikiwa huduma ya umeme, mtamfikiwa, kazi iliyo mbele yenu ni kusuka waya (Wiring) katika nyumba zenu, ili umeme utakapofika maeneo yenu, kazi iwe ni kuunganisha tu umeme kwenye nyumba zenu kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000.”
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa Wananchi wote wafikishiwe huduma ya umeme ili uwasaidie kujiletea maendeleo”. Amesema Naibu Waziri Kapinga.
Pili, niwahakikishie baada ya kufikisha umeme kwenye vijiji vyote, sasa tutaamia kwenye vitongoji na Serikali, imeshampata Mkandarasi, ambaye leo hii, nitamtambulisha mbele yenu, kazi yake itakuwa ni kusambaza umeme kwenye vitongoji 35 vya Jimbo lenu la Peramiho lakini pia atasambaza umeme kwenye vitongoji vyote 284 vya mkoa wote wa Ruvuma.”Alisema Kapinga.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri Kapinga alimkaribisha Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi, Musa David kutoka kampuni ya MF Electrical Engineering kuwasalimia Wananchi na baadae aliahidi kuanza kazi mara moja ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vya Jimbo la Peramiho na mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi mkoa wa Ruvuma kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Robert Dulle amesema kukamilika kwa Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) kwenye Jimbo la Peramiho pekee kumeigharimu Serikali kiasi cha shilingi milioni 149 huku mkoa wote wa Ruvuma, zikitumika bilioni zaidi ya 91 kusambaza nishati ya umeme kwenye vijiji vyote, kupitia Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) pekee.
Mhandisi Dulle ameongeza kuwa REA imefikisha nishati ya umeme kwenye vitongoji 1,917 huku vitongoji vilivyosalia vikiwa ni 1,776 sawa na asilimia 51.9.
Miradi mengine inayotekelezwa na REA katika mkoa wa Ruvuma ni pamoja na Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji; Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Migodi Midogo na Maeneo ya Kilimo na Mradi wa Ujazilizi 2 (C). Miradi hiyo yote, ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 54.