Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma ametembelea eneo la mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Arusha leo Julai 30, 2024 kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kushuhudia mkandarasi akiendelea na utekelezaji wa kazi mbalimbali.
Akiwa katika eneo la mradi huo, ameelezea kufurahishwa na dhamira ya dhati ya utekelezaji kwa vitendo wa maono ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kwa ajili ya AFCON 2027.
"Mkandarasi anajua tuko nyuma ya muda kidogo kwa hiyo ametuhakikishia kuwa atatekeleza jukumu hili Kwa kufidia muda ulipotea kwa ili kukamilisha mradi huu kwa wakati ili uweze kutumika kwa ajili ya AFCON" amesema Mhe. Mwinjuma
"Nimekuta pia wananchi wengi ambao wanapata ajira za moja kwa moja kwenye ujenzi wa mradi huu nao pia wako tayari sana na wanafanya kazi ambayo imewaleta hapa wakijua kuwa wanafanya kazi kwa ajili ya manufaa ya nchi" amesisitiza.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya CRCEG, Gregory Mbuya amesema mradi huo utatekelezwa kwa miezi 24 na tayari kazi za maandalizi zimeshaanza na zinaendelea vizuri.