Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amekiagiza Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kikae na Baraza la michezo la Taifa (BMT), kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya mchezo huo hapa nchini
Mhe. Mwinjuma ametoa agizo hilo alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa CHANETA leo Julai 30 2024 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa AICC Jijini Arusha.
Amesema katika kipindi cha miaka iliyopita mchezo huo ulikuwa namba mbili nchini kwa kupendwa na sasa umepoteza umaarufu na mvuto kwa sababu ya migogoro hali inayosababisha ukose wadhamini.
Kuhusu kuleta wataalamu wa mchezo huo ili kuwanoa wataalamu waliopo au kuwapeleka nje wataalamu hao, Mhe, Mwinjuma amesema Serikali italifanyia kazi suala hilo ili kupata wataalamu mbalimbali wakiwemo makocha na waamuzi kuendeleza mchezo huo hapa nchini.
Aidha Mhe, Mwinjuma amekisisitiza chama hicho kuepuka upendeleo wakati wa uchaguzi wa timu ya taifa na kusisitiza maandalizi ya kutosha ambayo yataiwezesha timu ya taifa ifanye vizuri na Serikali kutoa ruhusa kwa timu hiyo kuiwakilisha nchi pindi inaposhiriki michuano ya kimataifa
Awali Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania, (CHANETA), Dkt. Devotha Marwa, amesema lengo la mkutano Mkuu wa chama hicho ni kujadili maendeleo ya mchezo wa Netiboli nchini, kupitia Katiba ya CHANETA na kupokea taarifa ya fedha .